Syria yafichua njama za watawala wa nchi za Kiarabu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Miqdad amesema kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zimewapatia magaidi kiasi cha dola bilioni 137 kwa shabaha ya kuiharibu Syria.
Habari hizo zinazofichua mambo mbalimbali kuhusu mgogoro wa Syria zinawaelekeza walimwengu katika hakika kwamba, mgogoro huo ni matokeo ya njama zilizopangwa na nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu. Njama hizo za kigeni zilizoongozwa na Marekani, Israel, Saudi Arabia na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu zimeitumbukiza nchi hiyo katika vita vilivyochukua roho za maelfu ya watu wasio na hatia na kusababisha uharibifu mkubwa. Nchi hizo ziliparamia malalamiko ya wananchi katika baadhi ya maeneo ya Syria na kuanza kutuma makundi ya kigaidi nchini humo ambayo yamekuwa yakifanya uharibifu na mauaji ya kutisha kwa kipindi cha miaka saba sasa. Njama hizo za nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu zilifanyika katika fremu na mpango mpana zaidi wa kutaka kuzidhoofisha nchi za eneo la Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel na kuzigawa baadhi ya nchi ikiwemo Syria yenyewe. Mpango huo ulibuniwa na Marekani, Israel na washirika wao na kutekelezwa kwa fedha na silaha zilizonunuliwa na Saudi Arabia, Imarati na kadhalika.
Gazeti la Uingereza la Independent wiki kadhaa zilizopita lilifichua nyaraka zinazoonesha uhusiano mkubwa wa Saudi Arabia na makundi ya kigaidi na kiwango kikubwa cha misaada ya sihala ya nchi hiyo kwa makundi ya kigaidi nchini Syria. Nyaraka hizo zilionesha kuwa Saudi Arabia imekuwa ikinunua silaha kutoka nchi za Bulgaria, Serbia na Marekani na kuzipeleka kwa makundi ya kigaidi kama lile la Daesh nchini Syria. Mwandishi wa habari wa gazeti la Independent la Uingereza, Robert Fisk anasema kuwa, nyaraka hizo za manunuzi ya silaha na jinsi zilivyokuwa zikitumwa kwa makundi ya kigaidi zimepatikana katika makazi yaliyoharibiwa ya magaidi hao nchini Syria.
Saudi Arabia, Israel, Imarati na nchi nyingine kadhaa za Magharibi ndizo zinafadhili na kusuka mipango yote ya vita na machafuko ndani ya Syria. Nchi hizo zilikusudia kuiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo na kuhakikisha kwamba, zinapandikiza serikali na viongozi watakaotii na kutekeleza amri za mabwana zao kama walivyo baadhi ya watawala na wafalme wa nchi za Kiarabu na hivyo kulinda usalama wa dola haramu la Israel. Hata hivyo kusimama kidete kwa wananchi, serikali na jeshi la Syria na misaada ya waitifaki wa nchi hiyo kama Hizbullah, Iran na Russia kumekwamisha njama hizo.
Si hayo tu bali gharama kubwa za vita vya Syria na mabilioni ya dola yaliyotolewa na nchi za Kiarabu kufadhili makundi ya kigaidi katika kutekeleza njama na mipango ya Marekani na Israel sasa vimezitumbukiza baadhi ya nchi hizo za Kiarabu katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi.