Wairaqi wapinga kufunguliwa ubalozi mdogo wa Saudia huko Basra
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47584-wairaqi_wapinga_kufunguliwa_ubalozi_mdogo_wa_saudia_huko_basra
Wananchi wa mkoa wa Basra nchini Iraq wamefanya maandamano makubwa sambamba na kuenea tetesi kuhusu uwezekano wa kufunguliwa ubalozi mdogo wa Saudi Arabia katika eneo hilo.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Aug 21, 2018 07:47 UTC
  • Wairaqi wapinga kufunguliwa ubalozi mdogo wa Saudia huko Basra

Wananchi wa mkoa wa Basra nchini Iraq wamefanya maandamano makubwa sambamba na kuenea tetesi kuhusu uwezekano wa kufunguliwa ubalozi mdogo wa Saudi Arabia katika eneo hilo.

Tangu mwaka jana wa 2017 Saudi Arabia imeelekeza zaidi mazingatio yake kwa Iraq. Katika kipindi hicho Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Adel al-Jubeir ametembelea Iraq na kwa upande mwingine viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Iraq akiwemo Waziri Mkuu, Heidar al Abadi amefanya ziara nchini Saudi Arabia. Vilevile Saudia imefungua tena ubalozi wake mjini Baghdad baada ya kufungwa kwa kipindi cha miaka 27. Hata hivyo tunapochunguza mienendo ya Saudi Arabia tunaona kuwa, Riyadh imekuwa ikifanya njama za aina mbalimbali za kuingilia masuala ya ndani ya Iraq. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mwaka jana serikali ya Baghdad ikamtimua nchini humo balozi wa Saudi Arabia, Thamer al-Sabhan kwa sababu ya harakati zake za kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. al Sabhan alituhumiwa kuchochea machafuko ya ndani na kukutana na wanachama wa kundi la kigaidi la Baath. 

Thamer al-Sabhan

Saudi Arabia imeelekeza mazingatio yake katika suala la kufungua balozi ndogo katika maeneo mawili ya Basra na Kurdistan, suala ambalo linafichua njama za serikali ya Riyadh za kutaka kuingilia masuala ya ndani ya Iraq na kuzusha matatizo ya kiusalama. Katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni Saudi imefanya jitihada kubwa za kutaka kufungua ubalozi mdogo katika mji wa Basra. Januari mwaka huu balozi wa Saudia nchini Iraq, Abdul Aziz Khalid Shimmari alitangaza kuwa Baghdad imeafiki suala la kufunguliwa ubalozi mdogo wa Saudia katika mji wa Basra. 

Mtaalamu wa masuala ya kistratijia Hassan Shukripour anasema, hatua ya sasa ya Saudi Arabia ya kuelekeza mazingatio yake kwenye eneo la Basra ina sababu mbili kuu: Kwanza ni utajiri mkubwa wa mafuta wa eneo hilo na pili ni muundo wa kijamii wa mkoa wa Basra. Sehemu kubwa ya mafuta ya petroli ya Iraq inatoka katika mkoa wa Basra, na jamii karibu yote ya mkoa huo inaundwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia. 

Masjid Imam Ali (as) mjini Basra

Katika upande mwingine wakazi wengi wa mkoa huo wanalalamika kwamba, licha ya kwamba, sehemu kubwa ya utajiri wa mafuta wa Iraq inatoka katika mkoa huo lakini kiwango cha ukosefu wa ajira ni kikubwa sana katika eneo hilo. Wanasema makampuni ya kigeni yanayochimba mafuta katika eneo hilo yanafadhilisha kuwaajiri wafanyakazi wa kigeni kwa bei nafuu badala ya kuajiri nguvu kazi ya eneo hilo. Suala hilo limezidisha malalamiko ya wakazi wa Basra.

Saudi Arabia ambayo inaelewa vyema mazingira ya ndani ya Iraq inafanya njama za kutumia malalamiko hayo kwa ajili ya kuchochea machafuko na kuzidisha hali ya ukosefu wa usalama huko Basra na hatimaye kuzusha migawanyiko katika safu za Waislamu wa Kishia na baina yao na serikali kuu ya Baghdad. Kwa maneno mengine ni kuwa, Saudia inafanya mikakati ya kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya Mashia na kudhoofisha nafasi yao katika muundo wa kisiasa wa Iraq. Si hayo tu, bali Riyadh imekuwa ikinunua ardhi za kilimo katika mkoa wa Basra na kuwapa vibaraka na wafuasi wake.

Basra, Iraq

Kwa kutilia maanani hali hiyo wakazi wa mkoa wa Basra wanaoelewa vyema mipango na mikakati ya Saudi Arabia, wamefanya maandamano makubwa wakipinga suala la kufunguliwa ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Basra. Maandamano hayo sasa yamekwamisha shughuli za kufunguliwa ubalozi huo.