Syria yalaani ripoti ya Wamagharibi kuhusu silaha za kemikali
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelaani vikali taarifa ya pamoja ya Marekani, Ufaransa na Uingereza kuhusiana na tuhuma bandia dhidi ya Damascus kwamba, imetumia silaha za kemikali.
Tarehe 21 mwezi huu, nchi hizo zilitoa taarifa ya pamoja kwamba serikali ya Syria imetumia silaha hizo. Kufuatia taarifa hiyo, Alkhamisi ya jana Damascus ilitangaza kwamba, nchi za Marekani, Ufaransa na Uingereza zimeendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi, kwa mashambulizi vya vyombo vya habari yanayolenga kupotosha fikra za walimwengu. Taarifa hiyo imeongeza kwamba, Syria imekuwa ikilaani matumizi yoyote ya silaha za kemikali katika eneo lolote na chini ya mazingira yoyote yale na kwamba Damascus haina silaha hizo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesisitiza kwamba silaha hizo zinatumiwa na makundi ya kigaidi ambayo yanaungwa mkono moja kwa moja na nchi za Magharibi na baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati hususan Saudi Arabia. Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeendelea kusisitiza kwamba, katika siku za hivi karibuni Damascus ilizitaarifu pande kadhaa za kimataifa kwamba makundi ya kigaidi yanajiandaa kutumia gesi ya sumu katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Tuhuma za Marekani, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Syria kwamba imetumia silaha za kemikali zimetolewa baada ya duru rasmi kutangaza Alkhamisi ya jana kwamba kundi linalojulikana kama 'Helmeti Nyeupe' limeonekana likihamisha shehena ya gesi aina ya Chlorine katika mkoa wa Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.