Ombi la Bahrain la kuwa mwanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la UN; nembo ya jeuri ya Aal Khalifa
(last modified Wed, 05 Sep 2018 02:30:54 GMT )
Sep 05, 2018 02:30 UTC
  • Ombi la Bahrain la kuwa mwanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la UN; nembo ya jeuri ya Aal Khalifa

Utawala wa Bahrain unaotekeleza siasa za ukandamizaji nchini humo umeomba kuwa mwanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Abdullah al Dussari ametangaza kuwa Bahrain inagombea kuwa mwanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Al Dussari alitangaza habari hiyo katika kikao cha mabalozi wa nchi za Kiarabu kilichofanyika huko Bahrain. Utawala wa Bahrain unatoa madai kuhusu haki za binadamu katika hali ambayo Zaid Ra'ad al Hussein Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza siku kadhaa zilizopita katika kikao cha baraza hilo huko Geneva kuwa: Bahrain inaendelea kuwakandamiza wanaharakati wa masuala ya kiraia na imepasisha sheria nyingi za ukandamizaji wa haki za binadamu. Ra'ad al Hussein Ameongeza kuwa: Viongozi wa Bahrain wanalipiza kisasi kwa wananchi wanaopigania kuwa huru na wanawatambua raia hao kuwa maadui zao. 

Zaid Ra'ad al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN 

Utawala wa Aal Khalifa unakabiliana na kukandamiza maandamano na mijumuiko yoyote inayofanyika kwa amani nchini humo na kulipizaji kisasi kwa wapinzani wanaoupinga utawala huu ulioko madarakani. Tukitupia jicho utendaji wa utawala wa Aal Khalifa tunashuhudia rekodi nyeusi kuhusu haki za binadamu ya utawala huo. Bahrain ilikumbwa na maandamano ya wananchi ya kupigania haki zao na kupinga ukandamizaji wa utawala wa Manama tangu mwezi Februari mwaka 2011. Wananchi hao wamekuwa wakifanya maandamano ya amani wakitaka kuwa huru, kutekelezwa uadilifu, kukomesha ubaguzi, kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia na kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa. Hata hivyo serikali ya Bahrain inatumia siasa za mkono wa chuma na inawatia mbaroni, kuwafunga jela, kuwatesa na kuwanyang'anya uraia wapinzani katika harakati za kukabiliana na matakwa hayo halali ya wananchi.  

Maandamano ya amani ya wananchi wa Bahrain dhidi ya serikali

Bahrain imechukua uamuzi wa kugombea uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa licha ya kwamba ni moja kati ya nchi zinazokiuka pakubwa haki za binadamu katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla. Kwa msingi huo ili kufanikisha suala hilo, utawala wa ukoo wa Aal Khalifa una matarajio makubwa ya kupata misaada ya kifedha kutoka Saudia na kuzitumia kwa ajili ya kuzishawishi baadhi ya nchi  ziipigie kura na kuunga mkono ombi lake la uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu. Kuwepo kwa Bahrain pamoja na nchi kama Imarati na Saudi Arabia katika Baraza la Haki za Binadamu ambazo mbali na kukiuka waziwazi haki za raia wao, zinaendelea kumwaga damu za watu wasio na hatia katika nchi nyingine hususan huko Yemen, kunaweza kwa kiasi kikubwa kutia alama kubwa ya kuuliza kuhusu utendaji wa taasisi za Umoja wa Mataifa. 

Nukta ya kuzingatia ni kwamba, nchi za Magharibi zinazouunga mkono utawala wa Aal Khalifa zinajaribu kuficha jinai za utawala huo wa kidikteta kupitia mbinu mbalimbali. Katika fremu hii ofisi ya mwakilishi wa Umoja wa Ulaya huko Riyadh mwaka 2014 uliipatia Taasisi ya Taifa ya Haki za Binadamu yenye mfungamano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain tuzo iliyopewa jina la "Shaw" kwa ajili ya kuboresha haki za binadamu katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Himaya ya nchi za Magharibi kwa utawala wa Aal Khalifa unazifanya nchi hizo zitambulike kama waungaji mkono wa jinai zinazofanywa na utawala huo ulio dhidi ya binadamu. Himaya hiyo pia ndiyo inayoubakisha madarakani utawala wa kidikteta wa Bahrain, kuupa jeuri na kuuandalia uwanja na mazingira ya kujiunga na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.