Intifadha ya Quds yamtia kiwewe Netanyahu
Waziri Mkuu wa Utawala Haramu wa Israel ameshindwa kuficha wasiwasi wake kutokana na Wapalestina kuendeleza Intifadha ya Quds dhidi ya utawala wa Kizayuni
Benjamin Netanhayu ameashiria jambo hilo leo Jumapili katika kikao cha baraza la mawaziri wa utawala wa Kizayuni na kuzungumzia suala la walowezi wa Kizayuni kukosa usalama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu na kusema, hilo ni natija ya oparesheni za wanamapambano wa Palestina.
Netanyahu amesema, jeshi la utawala wa Kizayuni litazidisha oparesheni zake kwa lengo la kukabiliana na Intifadh ya Quds.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kuvuruga utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.
Wapalestina zaidi 200 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.