Jitihada za Hamas za kuhitimisha mzingiro Ukanda wa Ghaza
Afisa anayehusika na masuala ya uhusiano wa kimataifa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa harakati hiyo inafanya jitihada maalumu ili kuhitimisha mzingiro na kuifanya tulivu hali ya mambo huko Ghaza na kwamba hakuna upande unaoweza kupinga au kukabiliana na mchakato huo.
Usama Hamdan ameashiria hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa harakati hiyo inatoa zingatio maalumu kwa hali ya eneo hilo na haitaruhusu Ghaza kusambaratishwa.
Hamdan amesisitiza pia kuhusu mazungumzo ya Cairo akisema kuwa Misri imeualika huko Cairo ujumbe wa Hamas ili kufanya mazungumzo na viongozi husika wa nchi hiyo; hata hivyo mazungumzo hayo yanaonekana kudorora zaidi kuliko ilivyotarajiwa kutokana na ukwamishaji unaofanywa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Hamas ameashiria juhudi mbalimbali za kutatua vizuizi hivyo na kubainisha kuwa hakuna mtu pia anayeweza kuwa bega kwa bega na utawala wa Kizayuni katika kuizingira Ghaza halafu adai kuwa ni mzalendo.
Utawala wa Kizayuni umeliweka eneo la Ghaza chini ya mzingiro wa nchi kavu, anga na baharini tangu mwaka 2006; hatua iliyowasababisha matatizo chungu nzima wakazi wa eneo hilo.