Russia: Magaidi wapeleka Idlib matanki ya gesi ya kemikali
Msemaji wa kituo cha usitishaji vita cha Russia huko Syria amearifu kuwa magaidi wanajiandaa kuanzisha chokochoko dhidi ya raia wa Syria kwa kutumia mada za kemikali na kwamba tayari wamepelekea matanki yenye gesi ya klorini katika eneo la kiraia katika mkoa wa Idlib magharibi mwa Syria.
Vladimir Savchenko msemaji wa kituo cha usitishaji vita cha Russia nchini Syria ameeleza kuwa kundi la kigaidi la Jabhatul Nusra wamejiandaa kufanya shambulizi la mada ya sumu dhidi ya raia lengo likiwa ni kuituhumu Damascus kuwa imetumia silaha za kemikali.
Savchenko aliwahi kueleza pia kuwa televisheni kadhaa katika eneo la Mashariki ya Kati na kanali moja ya habari ya Marekani zimeelekea katika mji wa Jaisr al Shughur mkoani Idlib ili kupiga picha zinazohitajika kuhusu hujuma hiyo ya kichokozi ya magaidi ya kutumia silaha za kemikali dhidi ya Damascus. Tangu wiki tatu zilizopita hadi sasa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa taarifa mbalimbali ikitahadharisha kuhusu njama za magaidi za kutekeleza shambulio hilo la kemikali katika mkoa wa Idlib.
Wakati huo huo Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi pia zimeituhumu serikali halali ya Syria kuwa imeratibu mipango ya kutekeleza shambulio la kemikali huko Idlib na kuitahadharisha nchi hiyo.