Polisi ya Uturuki: Mwandishi habari, Khashoggi ameuawa katika ubalozi wa Saudia
Duru za kuaminika nchini Uturuki zimesema huenda mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud Jamal Khashoggi aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul Jumanne iliyopita ameuawa.
Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa, tathmini ya mwanzo ya Polisi ya Uturuki kwa sasa ni kuwa, Khashoggi ameuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul na kisha mwili wake ukatupwa nje ya ubalozi huo. Hata hivyo duru hizo za kiusalama hazijatoa maelezo zaidi kuhusu habari ya kuuawa mwanahabari huyo raia wa Saudia.
Vyombo vya usalama nchini Uturuki vinaitakidi kuwa, raia 15 wa Saudia ambao waliwasili nchini humo siku ambayo Khashoggi alitoweka na kisha siku hiyo hiyo wakaondoka na kurejea Riyadh, yumkini walihusika katika kutoweka na 'kuuawa' mwandishi huyo wa habari mkosoaji wa Aal-Saud.
Hapo jana Human Rights Watch ilisema kuwa, kutoweka kwa mwandishi habari na mkosoaji wa siasa za serikali ya Saudi Arabia, Jamal Khashoggi ambaye mara ya mwisho alikuwa katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, ni mgogoro mwingine wa haki za binadamu kwa serikali ya Riyadh.
Jina la Jamal Khashoggi lilikuwa katika orodha ya watu wanaosakwa kwa udi na uvumba na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na kwa msingi huo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema kuwa ametekwa nyara kwa amri ya Bin Salman.
Serikali ya Uturuki imemsaili balozi wa Saudia mjini Istanbul kuhusiana na kadhia ya kutoweka mwandishi huyo mashuhuri.