Rais Aoun: Serikali ya Lebanon kuundwa katika kipindi kifupi kijacho
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48883-rais_aoun_serikali_ya_lebanon_kuundwa_katika_kipindi_kifupi_kijacho
Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema serikali mpya ya nchi hiyo itaundwa katika kipindi kifupi kijacho.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 18, 2018 10:38 UTC
  • Rais Aoun: Serikali ya Lebanon kuundwa katika kipindi kifupi kijacho

Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema serikali mpya ya nchi hiyo itaundwa katika kipindi kifupi kijacho.

Rais Aoun ameyasema hayo leo mjini Beirut katika kikao na waandishi wa habari ingawaje hajaanisha serikali hiyo itaundwa kufikia lini.

Hata hivyo duru zilizo karibu na serikali ya nchi hiyo zimedokeza kuwa, yumkini serikali mpya ya Lebanon ikaundwa kufikia mwisho mwa wiki hii.

Waziri Mkuu mteule wa Lebanon, Saad Hariri siku ya Jumanne alisema mchakato wa kuunda serikali mpya umechukua muda mwingi zaidi ya matarajio kutoka na kutokubaliana pande hasimu za kisiasa, lakini alisisitiza kuwa serikali hiyo itaundwa ndani ya siku chache zijazo.

Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri

Uchaguzi wa Bunge la Lebanon ulifanyika tarehe 6 Mei mwaka huu. Muungano wa Muqawama unaoongozwa na Hizbullah ndio uliojinyakulia viti vingi zaidi, lakini kwa mujibu wa katiba ya Lebanon, Waziri Mkuu inapasa ateuliwe kutoka mrengo wa Waislamu wa Kisuni.

Kwa sababu hiyo, japokuwa idadi ya viti vya harakati ya Al-Mustaqbal imepungua katika bunge jipya, lakini Rais Michel Aoun wa Lebanon alimkabidhi tena Saad Hariri jukumu la kuunda baraza la mawaziri kwa sababu Al-Mustaqbal ndiyo iliyopata viti vingi zaidi kulinganisha na makundi mengine ya Kisuni.