Wazayuni wa Israel washambulia Msikiti wa al Aqsa, wauvunjia heshima
Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameshambulia na kuvunjia heshima Msikiti mtukufu wa al Aqsa na kibla cha kwanza cha Waislamu wote duniani.
Walowezi karibu 60 wa Kizayuni wakiandamana na maafisa 55 wa serikali ya Israel ambao walikuwa wakisindikizwa na jeshi la utawala huo mapema leo waliingia katika Msikiti wa al Aqsa kupitia mlango wa Maghariba na kuzunguka ndani ya msikiti huo na baadaye walifanya ibada zao makhsusi ndani ya msikiti huo.
Wazayuni wa Israel wamezidisha mashambulizi na uvamizi wa Msikiti wa al Aqsa ndani ya mwaka huu wa 2018. Walowezi wa Kizayuni wakiandamana na askari wa utawala ghasibu wa Israel wamekuwa wakivamia na kuvunjia heshima eneo hilo tukufu mara kwa mara kwa shabaha ya kuharibu utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na kupachika mahala pake nembo na alama za Kiyahudi.

Wakati huo huo jeshi la Israel limeshambulia maeneo ya Ukingo wa Magharibi na kuwatia nguvuni Wapalestina 16.
Takwimu zinazonesha kuwa, Wapalestina wasiopungua elfu 6 na mia tano wakiwemo watoto 300 wanashikiliwa katika magereza na jela za Israel.