Mafuriko Jordan yauwa watu wasiopungua 18, wengi wao ni watoto
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49047-mafuriko_jordan_yauwa_watu_wasiopungua_18_wengi_wao_ni_watoto
Watu wasiopungua 18 wengi wao wakiwa ni watoto wa shule na walimu wameaga dunia katika mafuriko ya ghafla wakati walipokuwa katika matembezi ya kishule karibu na Bahari ya Chumvi (Dead Sea) nchini Jordan. Mafuriko hayo yametajwa kuwa ni maafa makubwa zaidi kuwahi kuikumba Jordan katika miaka ya karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2018 04:26 UTC
  • Mafuriko Jordan yauwa watu wasiopungua 18, wengi wao ni watoto

Watu wasiopungua 18 wengi wao wakiwa ni watoto wa shule na walimu wameaga dunia katika mafuriko ya ghafla wakati walipokuwa katika matembezi ya kishule karibu na Bahari ya Chumvi (Dead Sea) nchini Jordan. Mafuriko hayo yametajwa kuwa ni maafa makubwa zaidi kuwahi kuikumba Jordan katika miaka ya karibuni.

Mkuu wa polisi ya Jordan, Brigedia Jenerali Farid al Sharaa ameiambia televisheni ya nchi hiyo kuwa, watu 34 wameokolewa katika oparesheni kubwa iliyohusisha helikopta za polisi na askari jeshi. Baadhi ya watu walionusuriwa katika mafuriko hayo wana hali mbaya na wengi walioaga dunia ni watoto wenye umri wa  chini ya miaka 14.

Msemaji wa ulinzi wa raia Kapteni Iyad al Omar amesema kuwa idadi ya waliopoteza maisha huwenda ikaongezeka.

Majeruhi wa mafuriko Jordan wakifikishwa hospitali

Mafuriko hayo ya ghafla yametokea Jordan baada ya mvua kali zilizonyesha nchini humo baada ya kumalizika msimu wa joto.

Wakati huo huo Omar Razzaz Waziri Mkuu wa Jordan amesema kuwa inaonekana kuwa shule hiyo ilikiuka miongozo ya Wizara ya Elimu inayozuia safari katika eneo la Bahari ya Chumvi kutokana na hali mbaya ya hewa. Ameahidi kufanyika uchunguzi ambao utawafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wote watakaopatikana na makosa.