Hamas yalaani kitendo cha Imarati cha kumkaribisha Abu Dhabi, waziri Mzayuni
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu cha kumkaribisha mjini Abu Dhabi waziri wa utawala wa Kizayuni ambao kila leo unawaua shahidi wananchi wasio na hatia wa Palestina ni kitendo cha aibu.
Miri Regev, waziri wa michezo na utamaduni wa Israel alitembelea Umoja wa Falme za Kiarabu siku ya Ijumaa akiongoza ujumbe wa michezo wa utawala wa Kizayuni, ikiwa ni ziara ya kwanza kabisa ya waziri wa Israel kuitembelea Imarati.
Waziri huyo wa michezo na utamaduni wa utawala wa Kizayuni wa Israel alitembelea pia msikiti mmoja mjini Abu Dhabi kwa mwaliko wa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Sheikh Mohammed bin Zayed Aal Nahyan.
Kituo cha upashaji habari cha Palestina kimemnukuu Sami Abu Zuhri, msemaji wa HAMAS akisema jana kwamba, ukubwa wa uchungu wa kukaribishwa kwa mapana na marefu ujumbe wa Wazayuni ulioongozwa na waziri wa michezo wa Israel huko Abu Dhabi Imarati haukadiriki hasa kutokana na namna Israel inavyowaua kikatili watoto wa Kipalestina.
Wimbi la kuweko uhusiano rasmi baina ya utawala wa Kizayuni na nchi za Kiarabu zinazopakana na Ghuba ya Uajemi limeshika kasi sana hivi sasa. Baadhi ya nchi kama Saudi Arabia zinatangaza waziwazi kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za Wapalestina wasio na hatia, ni muitifaki wake wa kiistratijia katika kile kinachodaiwa na ukoo wa Aal Saud kwamba eti ni kukabiliana na Iran katika eneo hili.