Rais Mahmoud Abbas: Mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne' hautafanikiwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i49430-rais_mahmoud_abbas_mpango_wa_marekani_wa_'muamala_wa_karne'_hautafanikiwa
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne' hautafanikiwa na kwamba, njama zilizoanza tangu kutolewa 'Tangazo la Balfour' mwaka 1917 zingali zinaendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2018 04:17 UTC
  • Rais Mahmoud Abbas: Mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne' hautafanikiwa

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne' hautafanikiwa na kwamba, njama zilizoanza tangu kutolewa 'Tangazo la Balfour' mwaka 1917 zingali zinaendelea.

Mahmoud Abbas amesema hayo katika hotuba yake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 14 tangu kuaga dunia Yasser Arafat aliyekuwa kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusisitiza kwamba, Beitul-Muqaddas na wakazi wake wote, asasi na maeneo yake matakatifu ya Kiislamu na Kikristo ni mji mkuu wa Palestina na kukiuka haki za wakimbizi wa Kipalestina ni jambo lisilokubalika.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kuwa, umoja ni silaha muhimu na imara zaidi kwa ajili ya kukabiliana na njama dhidi ya Palestina.

Aidha Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, mpango wa kulitenganisha eneo la Ukanda wa Gaza na ardhi za Palestina katu hautafanikiwa.

Maandamano ya kupinga mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne 

Kwa mujibu wa mpango wa serikali ya Marekani wa 'Muamala wa Karne', mji wa Beitul-Muqaddas utakabidhiwa kwa utawala haramu wa Israel, wakimbizi Wapalestina hawatakuwa tena na haki ya kurejea kwenye ardhi zao za asili na nchi ya Palestina itakuwa sehemu zilizobaki tu za ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

Kadhalika kwa mujibu wa mpango huo wa kidhalimu, mamlaka ya kusimamia msikiti mtukufu wa al-Aqsa zitakabidhiwa kwa pamoja Jordan, Palestina na utawala haramu wa Israel.