Abdollahian: Muqawama wa Wapalestina umewavunja moyo Wazayuni
Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu yuko katika ncha ya kuanguka, na kwamba muqawama wa Wapalestina umewavunja moyo Wazayuni.
Hossein Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, makundi ya wanaharakati wa Palestina yameuvunja moyo utawala huo ghasibu na kuufanya ujute, na ndiposa Netanyahu hivi sasa amejikuta katika njia panda.
Amir-Abdollahian aidha amelaani uvamizi wa hivi karibuni wa utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza, uliopelekea Wapalestina kadhaa kuuawa shahidi na wengine kujeruhiwa, sambamba na kuharibu majengo ya makazi ya watu na ofisi za kanali ya Al-Aqsa TV ya wanamuqawama.
Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ameashiria pia kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya jinai hizo dhidi ya Wapalestina na kusema kuwa, mashirika ya kimataifa yana wajibu wa kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina, kwa kulaani jinai za kinyama za Israel, katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu.

Itakumbukwa kuwa asubuhi ya Jumapili ya tarehe 11 Novemba, utawala huo ulifanya mashambulizi makali dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza ambapo kwa akali watu 13 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Katika jibu la hujuma hizo wanamuqawama wa Palestina walivurumisha karibu makombora 500 na kupiga vitongoji vya karibu na Gaza vya walowezi wa Kizayuni, ambapo idadi kadhaa ya Wazayuni waliangamizwa na kujeruhiwa; jambo lililoufanya utawala huo kulazimika kusitisha mara moja vita hivyo vya kichokozi, chini ya upatanishi wa Misri.