Wazayuni watoa wito wa kuuliwa kigaidi Mahmoud Abbas
Watu wasiojulikana wameanza kusambaza matangazo na kutundika makaratasi katika vituo vya upekezi vinavyodhibitiwa na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wakitaka kuuliwa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas.
Matangazo hayo yanayosambazwa kwa lugha ya Ebrania yanatoa wito wa kufanyika mauaji dhidi ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Hatua hiyo imechukuliwa sambamba na ripoti iliyotolewa jana na kanali ya 10 ya televisheni ya Israel ikimtaja Mahmoud Abbas kuwa ni kiongozi wa harakati ya PLO na kusisitiza kuwa, anasifu na kupongeza operesheni zinazofanywa na wanamapambano wa Palestina dhidi ya Wazayuni.
Wakati huo huo Mahmoud Abbas amelaani madai yanayoituhumu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kuwa ni kundi la kigaidi na kusema taifa la Palestina halitatambua rasmi mpango wa Muamala wa Karne na litaendelea kuisusia Marekani.
Katika mpango huo wa Muamala wa Karne uliobuniwa na Marekani na Israel na kubarikiwa na Saudi Arabia, Washington inataka kuanzishwa dola dhaifu la Palestina mji mkuu wake ukiwa kijiji cha Abu Dis, ambalo halitaruhusiwa kuwa na silaha. Vilevile mpango huo unapuuza kabisa haki ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika nchi yao na unaumilikisha kikamilifu utawala wa kizayuni wa Israel vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi vilivyojengwa na Israel katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu.