Palestina inahitaji dola milioni 350 za misaada ya kibinadamu: OCHA
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50245-palestina_inahitaji_dola_milioni_350_za_misaada_ya_kibinadamu_ocha
Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Isarel wanahitaji msaada wa dola milioni 350 mwaka 2019 kwa ajili ya huduma za kimsingi kama chakula, ulinzi, huduma za afya, malazi, maji na usafi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 18, 2018 03:25 UTC
  • Palestina inahitaji dola milioni 350 za misaada ya kibinadamu: OCHA

Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Isarel wanahitaji msaada wa dola milioni 350 mwaka 2019 kwa ajili ya huduma za kimsingi kama chakula, ulinzi, huduma za afya, malazi, maji na usafi.

Misaada hiyo inahitajika kwa Wapalestina milioni 1.4 wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Maghariki wa Mto Jordan.

Ombi hilo limezinduliwa Jumatatu mjini Ramallah na waziri wa maendeleo ya kijamii wa taifa la Palestina Dr Ibrahim Al-Shaer pamoja na  mratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu, OCHA; wa eneo hilo, Bw Jamie McGoldrick.

Waziri Al Shaer amesema,  hali ya kibinadamu katika eneo hilo inazidi kuzorota kutokana na kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi hizo na utawala wa haramu wa Israel.  Ameongeza kuwa, “tuna wasiwasi mkubwa kuhusu haki na huduma kwa watu maskini wanaohitaji msaada wa huduma za  kibinadamu.”

Hali mbaya katika Ukanda wa Ghaza

Kwa upande wake Bw McGoldrick, amesema hali inaendelea kuwa mbaya katika maeneo wanayoishi Wapalestina na hivyo kuwazuia  Wapalestina hao kupata huduma za afya, maji safi, maisha ya kawaida na mahitaji mengi mengine. Ameongeza kuwa, hii ni katika hali ambayo, wale watoao misaada wanakabiliwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kiwango kidogo cha ufadhili na ongezeko la mashambulizi  ili kuharamisha shughuli hizo za misaada.