Bunge la Palestina latupilia mbali uamuzi wa kulivunja uliotolewa na mahakama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50369-bunge_la_palestina_latupilia_mbali_uamuzi_wa_kulivunja_uliotolewa_na_mahakama
Naibu Spika wa Bunge la Palestina amesisitiza kuwa bunge hilo linapinga hukumu iliyotolewa na mahakama ya katiba ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuamuru bunge hilo livunjwe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2018 11:51 UTC
  • Bunge la Palestina latupilia mbali uamuzi wa kulivunja uliotolewa na mahakama

Naibu Spika wa Bunge la Palestina amesisitiza kuwa bunge hilo linapinga hukumu iliyotolewa na mahakama ya katiba ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuamuru bunge hilo livunjwe.

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, jana alitangaza kutekeleza uamuzi uliotolewa na mahakama ya katiba wa kulivunja bunge la Palestina.

Kwa mujibu wa televisheni ya al-Mayadeen, Ahmad Bahar, Naibu Spika wa Bunge la Palestina amesisitiza katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya katika Ukanda wa Gaza ya kwamba: Bunge la Palestina halikubaliani na uamuzi wa mahakama ya katiba wa kulivunja bunge hilo na litaendelea na shughuli zake kwa kujiamini na kwa uwezo kamili.

Ahmad Bahar, Naibu Spika wa Bunge la Palestina

Ahmad Bahar ameongeza kuwa: Bila kujali njama zinazofanywa, bunge hilo litaendelea kuunga mkono masuala ya kitaifa, muhimu zaidi ikiwa ni kadhia ya Quds, haki ya kurejea wakimbizi, kukombolewa mateka na maridhiano ya kitaifa.

Naibu Spika wa Bunge la Palestina amefafanua kwamba, uchaguzi wa bunge inapasa ufanyike wakati mmoja na uchaguzi wa rais wa Mamlaka ya Ndani na wa Baraza la Taifa la Palestina ili kulinda miundomsingi ya mfumo wa kisiasa wa Palestina.

Bunge la Palestina limepanga kufanya kikao maalumu siku ya Jumatano ijayo huko Ukanda wa Gaza, kujadili matokeo ya uamuzi huo uliochukuliwa na Mahmoud Abbas.../