Jan 05, 2019 07:46 UTC
  • Magaidi watwangana wenyewe kwa wenyewe Syria, mamia wauawa

Mamia ya magaidi wameangamizwa baada ya kuibuka mzozo miongoni mwa makamanda wa magenge hasimu ya kigaidi nchini Syria.

Kanali ya televisheni ya al-Mayadeen imeripoti kuwa, mtafaruku uliibuka baada ya genge la kigaidi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kuwashambulia magaidi wa kundi la Nour al-Din al-Zenki, kwa madai kuwa kundi hilo hasimu limeua wanachama wake watano, katika mkoa wa Aleppo (Halab).

Shirika linalodaiwa ni la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza na ambalo lina uhusiano wa karibu na magenge ya kigaidi nchini Syria la Syrian Observatory for Human Rights (SOHR) limethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mapigano hayo yaliyoanza tangu Jumanne hivi sasa yamesambaa hadi katika mikoa ya Idlib na Hama.

Habari zaidi zinasema kuwa, mapigano hayo yameshtadi hivi sasa hususan baada ya wapiganaji wa 'Jeshi Huru la Syria' wanaoungwa mkono na Uturuki kujitosa kwenye makabiliano hayo.

Magenge ya kigaidi nchini Syria

Haya yanajiri masaa machache baada ya Wizara ya Ulinzi ya Russia kusema kuwa, zaidi ya magaidi elfu 87 wameuawa katika mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya Syria, na kwamba 830 miongoni mwao walikuwa vinara na viongozi wa makundi ya kigaidi; mbali na vifaru 650 na zaidi ya magari 700 ya kivita ya magaidi hao kuteketezwa.

Mabaki ya magenge ya kigaidi nchini Syria hivi sasa yameonekana kuchanganyikiwa zaidi kufuatia tangazo la Rais Donald Trump wa Marekani la kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags