Jan 10, 2019 07:14 UTC
  • Ripoti: Wafungwa wa kisiasa Bahrain wana hali mbaya

Kituo cha Haki za Binadamu na Demokrasia nchini Bahrain kimetahadharisha kuhusu hali mbaya ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu waliofungwa katika jela za utawala wa Aal Khalifa nchini humo.

Kituo hicho kimelaani mateso wanayopewa wafungwa na kushikiliwa katika mazingira yasiyoridhisha katika Jela Kuu la al Jaw nchini humo na kuongeza kuwa, Ali al Haji na Naji Fateel, wafungwa wawili wa kisiasa walioko katika jela hiyo, siku kadhaa zilizopita waliteswa vikali kimwili na kiakili. 

Naji Fateel (L) na Ali Naji, wafungwa wa kisiasa wa Bahrain 
 

Kituo cha Haki za Binadamu na Demokrasia cha Bahrain kimewataka watawala wa nchi hiyo kushughulikia haraka iwezekanavyo hali ya wafungwa hao wa kisiasa.

Wakati huo huo Ali Haji na Naji Fateel wameandika barua kwa taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu ikiwemo Human Rights Watch wakitaka kuchukuliwe hatua za kimataifa ili kuushinikiza utawala wa Aal Khalifa kusitisha ukandamizaji dhidi ya wafungwa wa kisiasa. 

Makundi ya haki za binadamu yamekuwa yakilaani na kuukosoa utawala wa Manama kwa kuwakandamiza wapinzani na yametaka kufanyike marekebisho katika muundo wa kisiasa wa nchi hiyo. Vilevile Taasisi ya Kimataifa ya Sky Line yenye makao yake mjini Stockholm nchini Sweden mwaka jana iliripoti kesi 86 za ukiukaji wa haki za raia wa Bahrain unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa.   

Tags