Katibu Mkuu wa Arab League: Tutairejeshea Syria uanachama wake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50922-katibu_mkuu_wa_arab_league_tutairejeshea_syria_uanachama_wake
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amesema kuwa, licha ya kwamba suala la Syria ni tata kutokana na uingiliaji wa madola ya kigeni, lakini bila ya shaka yoyote Damascus itarejeshewa uanachama wake katika jumuiya hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2019 23:15 UTC
  • Katibu Mkuu wa Arab League: Tutairejeshea Syria uanachama wake

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amesema kuwa, licha ya kwamba suala la Syria ni tata kutokana na uingiliaji wa madola ya kigeni, lakini bila ya shaka yoyote Damascus itarejeshewa uanachama wake katika jumuiya hiyo.

Ahmed Aboul Gheit amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya DMC ya Misri na kusisitiza kwa kusema: "Tab'an kuandaliwa mazingira mazuri ndani ya Syria ni jambo muhimu katika ushirikiano wa nchi hiyo na Arab League."

Aidha amesema, serikali ya Rais Bashar al Assad kwa kushirikiana na waitifaki wake Russia na Iran imepata mafanikio mengi na kuweza kukomboa sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo, lakini uingiliaji wa madola ya kigeni kama vile Uturuki unaendelea kulitia utata suala la Syria.

Wanajeshi wa Syria wakisherehekea ushindi wakiwa wamebeba bendera za nchi yao pamoja na za Iran na Russia

 

Amma kuhusiana na uhusiano wa Iran na nchi za Kiarabu. Aboul Gheit amesema, ni jambo lisilo na shaka kwamba Iran ina marafiki zake kati ya nchi za Kiarabu na ndio maana Amr Mousa, Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu alipendekeza kupewa uanachama Iran na Uturuki katika jumuiya hiyo ili kuimarisha ushirikiano wa kieneo, tab'an baadhi ya wanachama wa Arab League walipinga pendekezo hilo.

Mwaka 2011 mara baada ya kuanza mgogoro wa ndani nchini Syria, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa mashinikizo makubwa ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Saudi Arabia iliamua kuipokonya Syria uanachama. Nchi nyingi za Kiarabu nazo zilifunga balozi zao na kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Syria. 

Hata hivyo na baada ya kushindwa njama zao, sasa hivi nchi za Kiarabu zinarejesha balozi zao, huku Imarati ikiwa ya kwanza kurejesha ubalozi wake mjini Damascus.