Siku ya Gaza, hatua athirifu katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina
Siku ya Gaza ambayo ni nembo ya kuwaunga mkono wakazi wa eneo la Gaza huko Palestina wanaokabiliwa na mzingiro imewadia katika hali ambayo, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Palestina imeshuhudia kuongezeka harakati za wananchi zenye lengo la kuuvunja mzingiro wa Gaza.
Siku ya Gaza ilibuniwa na kuanzishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lengo likiwa ni kuwaunga mkono wananchi wa Wapalestina. Kupewa jina la "Siku ya Gaza" tarehe hii ya 29 Dei ambayo mwaka huu imesadifiana na tarehe 19 Januari kumefanyika kwa shabaha ya kuthamini na kuenzi muqawama wa wananchi wa Palestina mbele ya vita vya siku 22 vya utawala haramu wa Israel na kuzuia kusahauliwa jinai za utawala huo ghasibu ulimwenguni sambamba na kufanyika juhudi za kutekelezwa uadilifu mkabala na utawala huo vamizi ambao umekuwa ukitenda jinai kila siku iendayo kwa Mungu.
Matukio ya Palestina kufuatia kupewa siku hii ya leo jina la Siku ya Gaza yanaonyesha kuweko mikakati na stratejia ya Iran ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika kalibu ya kutenga na kutangaza siku maalumu na kuzipatia majina kama vile Siku ya Quds na Siku ya Gaza. Hapana shaka kuwa, huu ni mwanzo wa matukio muhimu katika mapambano dhidi ya Uzayuni ya wananchi wa Palestina. Jambo hili linaonyesha kushindwa utawala huo ghasibu unaoikalia kwa mabavu Quds mwenendo ambao umekuwa ukiongezeka kila leo.
Ni katika kivuli cha matukio haya ndipo tunaposhuhudia kufanyika maandamano yenye anwani ya "Haki ya Kurejea na Kuvunja Mzingiro" katika mwaka mmoja uliopita huko Gaza ambapo duru ya 43 ya maandamano hayo ilifanyika jana Ijumaa ikiwa kubwa na yenye hamasa ya hali ya juu. Maandamano hayo yalifanyika kwa anwani ya "Kwa Kusimama Kidete Tutaushinda Mzingiro." Hii ni katika hali ambayo, duru ya 44 ya maandamano hayo imepangwa kufanyika wiki ijayo chini ya anwani ya "Jinai za Kuzingirwa Gaza, Njama Zisizosameheka". Kamati Kuu ya Kitaifa ya Maandamano ya "Haki ya Kurejea" na Kuvunja Mzingiro' katika miezi kadhaa iliyopita imefanya maandamano ya baharini pia lengo likiwa ni kuvunja mzingirio dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Kuendelea maandamano haya ya kupigania na kutetea haki za taifa la Palestina ni sisitizo la kuondolewa kikamilifu mzingiro wa kidhalimu dhidi ya Gaza na kutangaza upinzani dhidi ya "Makubaliano ya Karne." Maandamano ya kuondolewa mzingiro wa Gaza yanahesabiwa kuwa sehemu ya mlolongo mrefu wa mapambano ya wananchi wa Palestina. Mapambano na muqawama wa wananchi wa Palestina katika kipindi cha miaka 70 iliyopita umekuwa na nembo tofauti. Intifadha mbalimbali za Palestina ni miongoni mwa nembo za mapambano ya wananchi wa Palestina mkabala na utawala ghasibu wa Israel. Katika fremu hii, kile ambacho leo hii kinadhihirika katika mwenendo na mchakato wa mapambano dhidi ya Uzayuni ni kuwa, maandamano mbalimbali ya wananchi wa Palestina ni nembo ya muqawama wa kiraia kando ya muqawama na mapambano ya silaha dhidi ya wavamizi Wazayuni.
Wapalestina wakitegemea uwezo na nguvu mbalimbali za muqawama, kivitendo wamefungua uwanja mpya wa mapambano kwa ajili ya kukabiliana na njama dhidi ya Palestina. Harakati mbalimbali za malalamiko za Wapalestina katika Ukanda wa Gaza katika miezi ya hivi karibuni ni nukta muhimu katika mbinu ya mapambano ya Wapalestina ambayo inahesabiwa kama marhala na hatua mpya ya kimuqawama ya wananchi wa Palestina. Saadullah Zarii, mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya kati na Palestina anasema akitathmini stratejia ya Wapalestina, matunda na malengo yao kwamba:
Moja ya malengo haya ni kurejea hali ya kujikita walimwengu katika kadhia ya Palestina ambayo kutokana na matukio mengine ya eneo hili, ilikuwa imesahaulika.
Nukta ya kuzingatia katika uwanja huu ni kwamba, viongozi wa Palestina nao wamesisitiza juu ya kuweko mfungamano baina ya "Maandamano ya Haki ya Kurejea na kadhia ya "Siku ya Gaza". Hapana shaka kuwa, Siku ya Gaza ni kama injini athirifu katika kuleta hatua zaidi za himaya na na uungaji mkono kwa malengo matukufu ya Palestina. Ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuipa jina tarehe ya leo kuwa Siku ya Gaza, umekuwa na nafasi muhimu katika kuifanya jamii ya kimataifa izidi kuyaunga mkono malengo ya Palestina. Aidha hali hii imewafanya Wapalestina nao wawe na moyo maradufu wa kusimama kidete katika kuabiliana na wavamizi wa Kizayuni.