Makabiliano ya Saudia na Qatar nchini Sudan
(last modified Sun, 27 Jan 2019 11:52:18 GMT )
Jan 27, 2019 11:52 UTC
  • Makabiliano ya Saudia na Qatar nchini Sudan

Baada ya safari ya siku mbili ya Rais Omar al-Bashir wa Sudan mjini Doha, Qatar Mfalme wa Saudia pia alituma ujumbe huko Sudan ulioongozwa na mmoja wa mawaziri wake kwa ajili ya kukutana na al-Bashir.

Hatua ya Mfalme wa Saudia ya kutuma ujumbe Sudan, ni makabiliano ya wazi ya Riyadh dhidi ya Doha. Ukweli ni kwamba hali hiyo ina pande tatu ambazo ni Saudia, Qatar na Sudan. Ni tangu mwezi Juni 2017 ambapo Saudia imekata uhusiano wake na Qatar. Lengo la Saudia kukata uhusiano wake na Qatar, ni kuzidisha mashinikizo kwa serikali ya Doha ili kuifanya nchi hiyo ibadili siasa zake za kigeni na kufuata siasa za Riyadh. Hata hivyo kwa kipindi cha miezi 19 iliyopita si tu kwamba Qatar haijakubali kuwa chini ya udhibiti wa Saudia, bali imeonekana kuwa mshindi katika msuguano huo sambamba na kuutumbukiza utawala wa Aal-Saud katika changamoto nyingi zaidi kwa maslahi ya Doha. Sudan ni moja ya maeneo ya ushindani mkubwa kati ya Saudia na Qatar. Hii ni kusema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Sudan ilikuwa ikifuata siasa za Saudia na hata kufikia kushiriki katika vita vya Riyadh dhidi ya nchi masikini ya Yemen, hata hivyo Riyadh haikuweza kuivutia zaidi serikali ya Khartoum licha ya kutumia fedha nyingi katika suala hilo.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipowasili Qatar

Aidha katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya wananchi wanaolalamikia hali mbaya ya uchumi. Katika uwanja huo serikali ya Khartoum na kwa lengo la kuzima maandamano hayo, imeomba uungaji mkono wa kifedha kutoka nchi za kigeni ikiwemo Qatar. Katika fremu hiyo ndipo Rais Omar al-Bashir wa Sudan akafanya safari ya siku mbili nchini Qatar na kukutana na Tamim bin Hamad Al Thani, Amiri wa nchi hiyo ingawa hata hivyo hakupata mapokezi makubwa. Gazeti la Raialyoum limezungumzia suala hilo kwa kuandika: "Licha ya rais wa Sudan kuwa kiongozi wa kwanza wa Kiarabu kufanya safari nchini Qatar baada ya safari ya Mfalme wa Kuwait katika kipindi cha karibu miezi sita iliyopita, lakini hakupata mapokezi yenye uzito mkubwa katika uwanja wa ndege wa Doha, kwa sababu Mfalme Tamim bin Hamad Al Thani hakwenda kumlaki yeye mwenyewe; na badala yake kiongozi huyo alilakiwa na Waziri Mshauri katika masuala ya kigeni pamoja na balozi wa Sudan mjini Doha." Pamoja na hayo, hatua hiyo ya Rais Omar al Bashir ilitosha kumfanya Mfalme Salman wa Saudia, kutuma ujumbe unaoundwa na Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Waziri wa Usafirishaji na Waziri wa Masuala ya Nchi za Afrika kwenda Khartoum, Sudan kwa lengo la kukutana na rais wa nchi hiyo.

Tamim bin Hamad Al Thani, Mfalme wa Qatar ambaye anaonekana kumpiku Mfalme Salman wa Saudia

Shirika la habari la Saudia (WAS) limeelezea safari ya ujumbe huo kwamba: "Safari ya ujumbe wa Saudia imefanyika kupitia amri ya Mfalme wa nchi hiyo na kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuongeza mabadilishano ya kibiashara na Sudan." Wakati huo huo Majid bin Abdullah Al Qasabi, Waziri wa Biashara na Uwekezaji wa Saudia amesema kuwa: "Riyadh imetoa mkopo wa zaidi ya Dola bilioni 23 kwa ajili ya kuunga mkono miradi ya maendeleo nchini Sudan." Hatua hiyo ya mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia inaonyesha kwamba, ushindani uliopo na nchi ndogo ya Qatar ndio umemfanya atoe kiwango kikubwa cha fedha kwa Sudan kupitia kile kinachoitwa 'msaada wa kisiasa.' Aidha hatua hiyo ni ishara nyingine kwamba Mfalme Salman amepunguza mamlaka zaidi ya Mohammad Bin Salman, mwanaye na ambaye ni Mrithi wa Kiti cha Ufalme katika uga wa siasa za kigeni. Hii ni kwa sababu, mzozo uliopo na serikali ya Qatar na kadhalika hatua ya kujiweka mbali na Saudi Arabia nchi kadhaa kama vile Sudan, ni matokeo ya siasa mbovu za mwanaye huyo.

Tags