Israel yakerwa na Uholanzi kutambua Gaza, Quds kuwa asili ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51474-israel_yakerwa_na_uholanzi_kutambua_gaza_quds_kuwa_asili_ya_wapalestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeghadhabishwa na hatua ya Uholanzi ya kuwapa Wapalestina wanaoishi nchini humo haki ya kuorodhesha Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Mashariki mwa Quds (Jerusalem) kama maeneo walikozaliwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 11, 2019 04:12 UTC
  • Israel yakerwa na Uholanzi kutambua Gaza, Quds kuwa asili ya Wapalestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeghadhabishwa na hatua ya Uholanzi ya kuwapa Wapalestina wanaoishi nchini humo haki ya kuorodhesha Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Mashariki mwa Quds (Jerusalem) kama maeneo walikozaliwa.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Raymond Knops aliliambia Bunge la Wawakilishi lililoko mjini The Hague kwamba, uamuzi huo umechukuliwa kwa msingi kuwa, Uholanzi haitambui kuwa Israel ina mamlaka juu ya maeneo hayo.

Awali Wapalestina wanaoishi Uholanzi na ambao asili yao ni maeneo hayo matatu yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, walikuwa na machaguo mawili tu walipotakiwa kuarifisha pahala pao pa kuzaliwa, ama Israel au "Isiyojulikana". 

Hata hivyo sasa Wapalestina hao wanaoishi Uholanzi wako huru kuarifisha maeneo yao ya asili, iwe ni Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan au Quds Tukufu.

Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina nchini Uholanzi

Katika hali ambayo nchi 136 wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaitambua Palestina kama taifa huru, lakini aghalabu ya nchi za Ulaya zimekataa kulitambua taifa huru la Palestina, zikidai kuwa zinasubiri utekelezaji wa kile kinachoitwa 'Muamala wa Karne".

Hii ni katika hali ambayo, msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alisema hivi karibuni kuwa, mpango wowote ambao haulengi kuundwa nchi huru ya Palestina ambayo mji wake mkuu ni Quds Tukufu, hatima yake ni kushindwa tu.