Ansarullah yaafiki mpango wa kupeleka askari al Hudaydah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51641-ansarullah_yaafiki_mpango_wa_kupeleka_askari_al_hudaydah
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Siasa la Yemen Mahdi al-Mashat amekutana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo na kutangaza kuwa harakati ya Ansarullah imeafiki mpango wa kutumwa tena askari katika mji wa bandarini wa al Hudaydah.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 19, 2019 03:54 UTC
  • Ansarullah yaafiki mpango wa kupeleka askari al Hudaydah

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Siasa la Yemen Mahdi al-Mashat amekutana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya nchi hiyo na kutangaza kuwa harakati ya Ansarullah imeafiki mpango wa kutumwa tena askari katika mji wa bandarini wa al Hudaydah.

Hatua hiyo ya harakati ya Ansarullah ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Stockholm yaliyotiwa saini Disemba mwaka jana na azimio nambari 2450 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa makubaliano hayo pande zote husika zilipaswa kutayarisha mazingira bora ya kusitishwa vita na kutumwa misaada ya kibinadamu katika mji wa al Hudaydah. Makubaliano hayo pia yalitaka kuondoka wapiganaji wote katika mji huo. Azimio nambari 2450 la Baraza la Usalama pia lilipasisha makubaliano hayo.

Baada ya kupita karibu siku 40 tangu makubaliano ya Stockholm yalipopasishwa, Saudia Arabia na kibaraka wake, yaani serikali iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi, imekuwa ikikwamisha utekelezaji wake. Kwa sababu hiyo mkuu wa timu ya wasimamizi wa Umoja wa Mataifa huko al Hudaydah, Michael Lollesgaard tarehe 11 mwezi huu wa Februari alitoa pendekezo la kupelekwa tena askari wa Yemen katika mji huo. Lollesgaard amesema kuwa: "Mpango huo unajumuisha suala la kuanzishwa vizuizi vya usalama barabarani kwa ajili ya kusaidia operesheni za kugawa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa mji huo chini ya usimamizi wa askari wa kimataifa." 

Michael Lollesgaard

Mwafaka wa harakati ya Ansarullah kuhusu utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango huo kwa mara nyingine unaonesha kuwa, harakati hiyo na waitifaki wake hawapokee amri kutoka nje ya Yemen, na kwa upande mwingine unaakisi irada na azma kubwa ya harakati hiyo ya kutaka kukomesha kabisa mgogoro wa ndani nchini Yemen. Hatua hii ya harakati ya Ansarullah ni kinyume kabisa na ile ya serikali iliyojiuzulu na kukimbilia Riyadh ambayo inapata amri na maagizo kutoka kwa utawala wa Saudi Arabia. Kwa sababu hiyo haina azma ya kweli ya kukomesha mgogoro wa ndani nchini Yemen kwani kwa mtazamo wa Saudia, kumalizika mgogoro huo kunawezekana tu kwa kurejea tena harakati ya Ansarullah katika hali yake ya kabla ya Septemba 2014. Kabla ya Septemba 2014 harakati ya Ansarullah ilikuwa imetengwa na kuwekwa kando kabisa kisiasa nchini Yemen na ilitambuliwa na serikali zilizokuwa zikitawala mjini Sanaa kama kundi lisilotakikana. 

Baada ya hapo na kadiri muda ulivyopita Ansarullah ilibadilika na kuwa harakati yenye nidhamu na utaratibu unaokubalika zaidi wa kisiasa nchini Yemen na kuwa nguzo muhimu ya taifa hilo.

Kiongozi wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah, Abdul-Malik Badreddin al-Houthi

Kwa kutilia maanani hali hiyo, haitarajiwi kwamba Saudi Arabia na vibaraka wake watakubaliana na mpango wa mkuu wa timu ya Umoja wa Mataifa inayosimamia amani huko al Hudaydah ya kurejesha tena wapiganaji katika mji huo kwa ajili ya kusaidia zoezi la kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia walioathiriwa na vita. Na hata kama watakubaliana nao basi watafanya jitihada za chini kwa chini za kupindisha au kukwamisha utekelzaji wake kamili. Mafanikio hayo ya harakati ya Ansarullah nchini Yemen yameufanya utawala wa kizazi cha Aal Saud huko Riyadh kumuuzulu Brigedia Jenerali Aboud al Shahrani ambaye alikuwa kamanda wa kikosi cha Mfalme Abdul Aziz na makamu wake kutokana na kushindwa mtawalia mbele ya jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah. 

Maiti za askari wa Saudia wanaoendelewa kuuawa nchini Yemen

Ukweli ni kwamba, Saudi Arabia, serikali iliyojiuzulu na kukimbilia Riyadh ya Yemen na madola ya kigeni yanayowaunga mkono katika vita dhidi ya taifa la Yemen hawataki kuona harakati ya Ansarullah ikiwa na nafasi muhimu katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo licha ya kukiri kwamba, imejiweka katika nafasi bora zaidi kisiasa na kijeshi ikilinganishwa na kabla ya vita vya miaka mine sasa vya Wasaudia na waitifaki wao.