Syria yaapa kulikomboa eneo la Idlib kutoka kwenye makucha ya magaidi
Mshauri wa Masuala ya Kisiasa na Vyombo vya Habari wa Rais wa Syria amesema kuwa, eneo la Idlib litakombolewa na Rais Recep Tayyep Erdogan hawezi kuunda ukanda eti wa amani huko kaskazini mwa Syria.
Bouthaina Shaaban ameongeza kuwa, haiwezekana kubakisha makundi ya kigaidi katika eneo la Idlib na hapana shaka kuwa, eneo hilo litakombolewa. Syria pia imekuwa ikisisitiza kwamba, Damascus haiwezi kuruhusu mkoa wa Idlib uliko kaskazini magharibi mwa Syria uwe maficho mapya ya makundi ya kigaidi. Syria inasisitiza kuwa, eneo hilo litakombolewa na kuondoka katika makucha machafu ya makundi ya kigaidi.
Mkoa wa Idlib unahesabiwa kuwa ngome ya mwisho kabisa ya makundi ya kigaidi yaliyovamia ardhi ya Syria kwa msaada wa nchi za Magharibi na washirika wao wa kikanda kama Saudi Arabia. Juhudi zinazofanywa na jeshi la Syria na washirika wake za kutaka kukomboa eneo hilo zimekuwa zikikwamishwa na muungano wa nchi za Kiarabu na Kimagharibi zikiongozwa na Marekani kwa kutumia visingizio vya aina mbalimbali kwa shabaha ya kubakisha maficho ya magaidi katika eneo hilo. Uturuki kwa upande wake imekuwa ikitumia siasa za kuuma na kupuliza katika kadhia hii. Kwa mfano tu mwaka 2017 nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki zilitia saini makubaliano ya kuanzisha maeneo ya amani katika mikoa ya kaskazini mwa Syria. Uturuki kama moja kati ya nchi hizo ilituma jeshi katika maeneo hayo kwa shabaha ya kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo. Hata hivyo picha za satalaiti zinaonesha kuwa, jeshi hilo la Uturuki limekuwa likiingia katika mkoa wa Idlib kwa uratibu na ushirikiano wa kundi la kigaidi la Jabhatu Nusra lililowekwa katika orodha ya makundi ya kigaidi ya kimataifa. Hatua hii ya jeshi la Uturuki ya kushirikiana na kundi la kigaidi la Jabhatu Nusra katika maeneo ya Idlib ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kupunguza machafuko yaliyotiwa saini huko Astana nchini Kazakhstan. Hatua hii ya Uturuki inatengeneza ukanda wa amani karibu na maficho salama kwa makundi ya kigaidi, suala ambalo linapingana na makubaliano ya Sochi yanayosisitiza udharura wa kuangamizwa makundi yote ya kigaidi.
Katika mazungumzo yao ya mwezi Septemba mwaka jana huko Sochi, Marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyep Erdogan walikubaliana kuanzisha operesheni za jeshi katika eneo la Idlib kwa ajili ya kulinda uhai wa raia na kuanzisha eneo lisilo la kijeshi katika mkoa huo ili kuwezesha ukombozi wa Idlib kutoka kwenye makucha ya magaidi bila ya madhara makubwa. Baada ya makubaliano hayo, Rais Putin wa Russia alitangaza habari ya kuanzishwa eneo la raia lenye ukubwa wa kilomita 15 hadi 20 katika eneo linalotenganisha baina ya jeshi la taifa la Syria na wapiganaji wa makundi ya kigaidi katika mkoa wa Idlib. Hata hivyo magaidi hao, waungaji mkono na wafadhili wao wameendelea kukwamisha utekelezaji wa mpango huo, na kivitendo wamelifanya eneo la Idlib kuwa ghala kubwa la silaha kwa kuendelea kutuma zana za kijeshi kwa makundi hayo ya kigaidi. Ripoti mbalimbali zinasema kuwa, maelfu ya wapiganaji wa makundi ya kigaidi raia wa nchi 60 duniani ambao wametimuliwa katika maeneo mbalimbali ya Syria, sasa wamejikusanya katika mkoa wa Idlib na Jarabulus.
Alaa kulli hal, misimamo imara ya serikali ya Syria inaonesha kuwa, nchi hiyo haitazembea hata kidogo katika suala la kukomboa maeneo yote ya nchi hiyo na katika uwanja huo haitafumbia jicho suala la kukomboa maeneo yote ya mkoa wa Idlib bila ya kujali ni kundi au nchi gani iliyotuma majeshi au wapiganaji katika eneo hilo. Hii ni sehemu ya stratijia ya serikali ya Rais Bashar Assad ya kuhakikisha inakomboa na kulinda ardhi yote ya Syria.
Inatupasa pia kusisitiza hapa kwamba, mbinu zinazotumiwa na nchi za Maghaibi hususan Marekani na vibaraka wake wa Kirabu hususan Saudi Arabia zimedhihirika wazi kwa watu wote na haziwezi tena kuzuia serikali ya Syria kukomboa maeneo yote yanayoshikiliwa na makundi ya kigaidi yanayofanyakazi au kupigana vita kwa niaba. Jambo jingine la kuashriwa hapa ni kuwa, sambamba na kutwangwa makundi ya kigaidi kama Daesh huko Iraq na Syria, wafadhili na waungaji mkono wao pia wamefeli na kushindwa kubadili mlingano wa kisiasa na kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati kwa maslahi ya waitifaki wao.
Inaonekana kuwa, zama za Marekani kutunisha kifua katika eneo hilo zimepita na uhakika huo unaonekana waziwazi katika maamuzi ya viongozi wa serikali ya Washington ambao sasa wamelazimika au kulazimishwa kuondoa sehemu kubwa ya majeshi ya nchi hiyo huko Syria baada kufeli kwa siasa zao za kijuba na kibeberu.