Riyadh al-Maliki: Hali ya Palestina ni ya maafa makubwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina amesema hali ya mambo huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni ya maafa na ametaka Umoja wa Mataifa uchukue hatua za kufuatilia ukiukaji haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Riyadh al-Maliki ameyasema hayo mjini Geneva katika mazungumzo na Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa. Amefafanua kuwa hali ya haki za binadamu huko Palestina ni mbaya sana kutokana na jumuiya za kimataifa kutosheka na utoaji taarifa tu badala ya kuchukua hatua za maana za kukomesha ukaliaji ardhi kwa mabavu na ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Al-Maliki amebainisha kuwa, ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na utawala wa Kizayuni sasa umekuwa suala la kudumu na la kuendelea kutokana na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo haramu na vile vile kwa kutochukuliwa hatua zozote za kisheria dhidi ya askari wa Israel na walowezi wa Kizayuni.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina ameashiria pia hali ya Ukanda wa Gaza na kutochukuliwa hatua yoyote na jamii ya kimataifa ya kukomesha mzingiro wa mwaka wa 12 sasa uliowekwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo hilo.
Riyadh al-Maliki amezungumzia pia jinai za kivita zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi unazozikalia kwa mabavu na kusisitizia ulazima wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuingilia kati suala hilo kwa ajili ya kukabiliana na ukiukaji haki za raia wa Palestina hasa watoto wadogo unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.../