Palestina yataka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi
-
Riyad Mansour
Mwakilishi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kutekeleza majukumu yake na kuzuia ujenzi wa vitongoji zaidi vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Riyad Mansour amewatumia ujumbe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na China ambayo ni Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama la umoja huo, akisisitiza udharura wa uungaji mkono wa kimataifa kwa wananchi wa Palestina kwa mujibu wa sheria za kibinadamu. Katika ujumbe huo Mansour ameashiria ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa unaoendelea kufanywa na Israel hususan ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina na kutoa wito wa kusitishwa mwenendo huo.
Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema licha ya jamii ya kimataifa kuutaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe ujenzi wa vitongoji hivyo katika ardhi ya Palestina lakini Israel imezidisha mara tatu kasi ya ujenzi katika maeneo hayo.
Israel inaendelea kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayoitaka kukomesha ujenzi wa vitongoji vya Wayahudi katika ardhi ya Palestina ikiungwa mkono na madola ya Magharibi hususan Marekani.