Mapigo ya makombora ya Wapalestina katika kujibu mashambulio ya Israel
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimethibitisha habari ya mashambulio ya makombora mawili ya Wapalestina yaliyovurumishwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelelekea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Kufuatia uvurumishaji wa makombora hayo sauti za ving'ora zimesikika katika vitongoji hivyo vya walowezi wa Kizayuni. Jibu hilo la makombora limetolewa baada ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel kulenga nyumba za Wapalestina wanaoshi katika Ukanda wa Gaza na kuua idadi nyingine ya raia Wapalestina wasio na hatia. Mapigo hayo ya makombora kutoka Gaza kuvilenga vituo vya Wazayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu bila shaka ni thibitisho la wazi kwamba wanamapambano wa Kipalestina wameimarisha uwezo wao wa kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni. Matukio ya Palestina yanaonyesha kuwa licha ya kuzidishwa hatua za ukandamizaji na unyama wa utawala huo haramu kwa lengo la kudhoofisha na hatimaye kuyafuta kabisa makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina, lakini nguvu za kijeshi za makundi hayo likiwemo la Hamas, zimekuwa zikiimarika kila siku licha ya kuzingirwa kwa pande zote Ukanda wa Gaza na maghasibu wa Kizayuni, jambo ambalo limewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa utawala huo. Kilele cha mashambulio hayo ya makombora ya Wapalestina katika kujibu uchokozi wa mara kwa mara wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, kilitimia Novemba mwaka uliopita wa 2018 ambapo mamia ya makombora yalivurumishwa kutoka ukanda huo kuelekea ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.
Mashambulio hayo yaliupelekea utawala huo kushindwa kijeshi katika kipindi cha siku mbili pekee. Kufuta kabisa mapambano ya Wapalestina pamoja na silaha zao ni moja ya malengo makuu ya utawala huo haramu unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, lakini lengo hilo kama yalivyo malengo mengine ya utawala huo, yamebakia kuwa ndoto tu kutokana na mapambano makali yanayoonyeshwa na Wapalestina. Maonyesho hayo ya nguvu kubwa ya mapambano ya Palestina na ambayo inaendelea kuimarika kila siku katika Ukanda wa Gaza, bila shaka yanatoka na uungaji mkono mkubwa wa wanachi kwa mapambano hayo ya Kiislamu. Kuhusu suala hilo, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Kiislamu ya Palestina Hamas, ameutahadharisha utawala wa Kizayuni dhidi ya kuchukua hatua yoyote ya kichochezi na ya kichokozi katika Ukanda wa Gaza. Ismail Hania amesema kwamba, iwapo Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel atafanya uchokozi mwingine katika Ukanda wa Gaza, atalipa gharama kubwa ambayo huenda ikamwangusha kisiasa.
Amesisitiza kwamba hakuna tofauti yoyote kwa Wapalestina kuhusu ni nani atakayekuwa waziri mkuu wa Israel kwa sababu wote wameazimia kumwaga damu ya Wapalestina wasio na hatia. Ismail Hania amesema kuwa siri ya nguvu ya Wapalestina dhidi ya utawala katili wa Israel katika miaka michache iliyopita na hasa katika miezi ya hivi karibuni, ni makombora yao na kuongeza kuwa ni kutokana na nguvu hiyo ndipo utawala huo haramu ukawa hauthubutu tena kufanya mashambulio makubwa dhidi ya Wapalestina kama ilivyokuwa kawaida katika miaka ya huko nyuma. Nguvu hiyo kubwa ya makombora ya Wapalestina ndiyo imeupelekea utawala huo kujizingira kwa ukuta, jambo linalothibitisha wazi kwamba umeshindwa kabisa kufikia ndoto yake ya kuendelea kujipanua katika ardhi za Waarabu na Waislamu. Gazeti la Misri la al-Ahram pia limeashiria hali hiyo ya udhaifu wa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa utawala huo hauna tena uwezo wa kuendelea kukabiliana na makundi ya mapambano ya Kiislamu kama vile Hizbullah ya Lebanon na mengine ya Palestina kwa sababu unaelewa vyema kwamba kama utaingia katika vita na makundi hayo basi unapasa kukubali hasara kubwa utakayoipata.
Hivi karibuni pia mtandao wa Kizayuni wa Debka ulitoa ripoti ukikiri kuwa 'ngao ya chuma' ya utawala huo haina tena uwezo wa kukabiliana na makombora ya makundi ya mapambano ya Kiislamu. Jeshi la utawala huo pia katika ripoti yake ya kila mwaka limekiri kuwa mwaka uliopita wa 2018 makombora na mizinga zaidi ya 1000 ilirushwa katika maeneo ya Wazayuni kutokea Ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa gazeti la Jerusalem Post, jeshi la Israel limesema kuwa kati ya makombora1000 yaliyorushwa na Wapalestina, ni makombora 200 pekee ndiyo yaliweza kuharibiwa na 'ngao hiyo ya chuma' na kwamba mengine yote yaliweza kulenga shabaha zilizokusudiwa. Matukio hayo ya Palestina bila shaka yanaashiria kuongezeka kwa nguvu ya Wapalestina ya kumzuia adui kuanzisha mashambulizi na vilevile uwezo wao wa kulenga shabaha za Wazayuni.