Dunia yaendelea kumpinga Trump kuhusu miinuko ya Golan ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i52415-dunia_yaendelea_kumpinga_trump_kuhusu_miinuko_ya_golan_ya_syria
Viongozi mbalimbali wa dunia wameendelea kutoa radiamali kali ya kupinga tangazo la urasimishaji la Rais Donald Trump wa Marekani kwa miinuko ya Golan ya Syia kwamba ni milki ya utawala haramu wa Kizayuni Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 26, 2019 10:03 UTC
  • Dunia yaendelea kumpinga Trump kuhusu miinuko ya Golan ya Syria

Viongozi mbalimbali wa dunia wameendelea kutoa radiamali kali ya kupinga tangazo la urasimishaji la Rais Donald Trump wa Marekani kwa miinuko ya Golan ya Syia kwamba ni milki ya utawala haramu wa Kizayuni Israel.

Katika uwanja huo Rais Michel Aoun wa Lebanon amelaani vikali hatua hiyo ya kutambua rasmi Miinuko ya Golan kuwa milki ya utawala huo bandia na kuongeza kwamba, rais wa nchi moja hana haki ya kuichukulia maamuzi nchi nyingine. Rais Aoun amesisitiza kwamba kitendo hicho cha Trump kinakinzana na sheria za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait pia imetoa taarifa ya kulaani hatua hiyo ya Trump na kusema kuwa itapelekea kusimama kwa mwenendo wa amani katika eneo la Asia Magharibi kama ambavyo pia ni tishio kwa usalana na uthabiti wa eneo hilo. Aidha wizara hiyo ya Kuwait imesisitiza kwamba miinuko ya Golan ni sehemu ya ardhi ya Syria na kwamba hatua hiyo ya rais wa Marekani ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Wakati huo huo Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Ismail Haniyeh amesema kuwa miinuko ya Golan itaendelea kusalia kuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa na Syria. Haniyeh ameyasema hayo katika radiamali yake kwa uamuzi huo wa kichochezi wa Trump na kuongeza kwamba mipango mipya ya Marekani dhidi ya eneo hili inazidi kubainika na sasa haki ya Syria ndio ya kwanza kulengwa. Kadhalika Mkuu huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesisitiza kwamba misimamo na njama hizo za kidhalimu za Marekani, katu haziwezi kubadilisha ukweli wa kihistoria na kijografia wa ardhi za Palestina na Syria katika miinuko ya Golan. Aidha ameongeza kwamba Harakati ya HAMAS itaendelea kusimama pamoja na Syria dhidi ya njama hizo za Marekani. Miinuko ya Golan ya mkoa wa Quneitra nchini Syria ilikaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Kizayuni mwaka 1967 katika vita vya siku sita kati ya Wazayuni hao vamizi na nchi za Kiarabu. Mwaka 1982 utawala huo katili uliitangaza miinuko hiyo kuwa ni sehemu ya milki yake, jambo ambalo limekuwa likipingwa na dunia nzima.