Amiri wa Qatar aondoka ghalfa katika kikao cha nchi za Kiarabu
(last modified Sun, 31 Mar 2019 14:43:46 GMT )
Mar 31, 2019 14:43 UTC
  • Amiri wa Qatar aondoka ghalfa katika kikao cha nchi za Kiarabu

Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani leo Jumapili ameondoka ghalfa katika kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) mjini Tunis, Tunisia.

Kikao hicho kilikuwa kimewaleta pamoja kwa mara ya kwanza watawala wa Saudi Arabia na Qatar tokea mgogoro wa kidiplomasia uliopoanza Juni mwaka 2017 baina ya Qatar na Saudi Arabia pamoja na waitifake wake.

Shirika la Habari la Qatar, QNA, limesema Sheikh Tamim aliondoka Tunisia baada ya kuhudhuria kikao cha ufunguzi cha mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Hakuna sababu yoyote iliyotajwa kuhusu uamuzi huo wa Amiri wa Qatar.

Picha wakati wa ugunzui wa mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Tunis

Kikao cha 30 cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kimeanza leo Jumapili nchini Tunisia katika hali ambayo karibu nusu ya viongozi wa nchi muhimu za Kiarabu hawajashiriki.

Kati ya viongozi ambao hawajaonekana katika kikao cha leo ni Rais Omar al Bashir wa Sudan, Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria, Sultan Qaboos wa Oman, Mfalme wa Bahrain Hammad bin Issa Aal Khalifa, Mfalme  Mohammad wa Sita wa Morocco na Khalifa Bin Zayed Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu na sasa Amiri wa Qatar  ni kati ya viongozi muhimu wa nchi za Kiarabu ambao hawako katika mkutano huo wa Tunis.

Tags