Arab League: Mauaji ya kimbari ya Israel Gaza yanalenga kuwatimua Wapalestina
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imelaani operesheni za mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kuzitaja hatua hizo kuwa ni sehemu ya mpango mpana kuwatimua kwa lazima Wapalestina wa eneo hilo.
Ahmad Abul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amelaani operesheni zinazoendelea za utawala wa Kizayuni katika eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza hususan katika eneo la Jabalia na kusema: Israel inatumia mwanya wa kushughulishwa na jinai za kimataifa huko Lebanon kwa kuongeza. uhalifu zaidi kwa rekodi yake ya aibu huko Gaza.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ameongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia siasa za kikatili mno kwa kuzuia kuingizwa kwa huduma muhimu kama vile maji na chakula kwa wakazi na kulenga vituo vya matibabu na kuharibu kabisa majengo.
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika kukabiliana na jinai mpya iliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika kambi ya Jabalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, imetoa taarifa na kueleza kuwa, mauaji ya utawala huo ghasibu katika kambi hiyo ni kuwaadhibu wakazi wa eneo kwa kusimama kidete na kupinga juhudi za utawala wa Kizayuni za kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao.
Utawala wa Kizayuni unaendelea kuidhalilisha jamii ya kimataifa na kupuuza maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kuutaka usimamishe vita mara moja na pia amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya kuutaka uchukue hatua za kuzuia mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza.
Idadi ya mashahidi katika Ukanda wa Gaza imefikia watu elfu 42,175 na waliojeruhiwa 98, 336 tangu kuanza kwa oparesheni ya kimbunga cha Al-Aqswa.