HAMAS: Uamuzi wa Iran kuhusu JCPOA ni wa kishujaa
Mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS) nchini Lebanon amesema kuwa, hatua ya Iran ya kusitisha kwa muda utekelezaji wa ahadi zake katika baadhi ya vipengee vya mapatano ya nyuklia ya JCPOA, inaonyesha kuwa ni maamuzi ya kishujaa.
Ahmad Abdul-Hadi ameyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Habari la IRNA na kuongeza kwamba uamuzi mwingine uliochukuliwa na Iran siku chache zilizopita kama vile wa kuwataja askari wa Kimarekani waliopo eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) kuwa ni magaidi, nao pia umeonyesha ushujaa na hali ya kujiamini ya Tehran mbele ya Marekani. Aidha Mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS) nchini Lebanon amesisitiza kwamba uamuzi huo wa Iran unaweka wazi uhalali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Abdul-Hadi pia amekitaja kitendo cha Marekani kuutaja mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni na pia uamuzi wake wa kuitambua miinuko ya Golan ya Syria kuwa mali ya utawala huo, kuwa ni hatua zisizo na thamani yoyote. Aidha amezungumzia msimamo wa muqawama wa Palestina katika kutoa jibu kali kufuatia uchokozi wa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, muqawama umejiweka tayari kwa ajili ya kujibu hujuma za utawala wa Kizayuni kwa kujibu mashambulizi kwa mashambulizi na damu kwa damu.