Wapalestina waungana kupinga 'Muamala wa Karne'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53407-wapalestina_waungana_kupinga_'muamala_wa_karne'
Katika hali ambayo 'Muamala wa Karne' bado haujazinduliwa rasmi, lakini kila mara wakati vyombo vya habari vinapofichua sehemu ya muamala huo, makundi ya Palestina huonyesha umoja katika kuupinga mpango huo wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2019 03:10 UTC
  • Wapalestina waungana kupinga 'Muamala wa Karne'

Katika hali ambayo 'Muamala wa Karne' bado haujazinduliwa rasmi, lakini kila mara wakati vyombo vya habari vinapofichua sehemu ya muamala huo, makundi ya Palestina huonyesha umoja katika kuupinga mpango huo wa Marekani.

Moja ya stratijia muhimu zaidi za utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi ni mpango wa 'Muamala wa Karne'.  Mpango huo unapendelea upande mmoja wazi wazi na ni kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel huku Wapalestina wakiwa ni wenye kupata hasara kubwa zaidi.

Katika mpango huo wa 'Muamala wa Karne' si tu kuwa suluhisho la serikali mbili halijazingatiwa, bali hata sehemu kubwa ya ardhi za Palestina ambazo zinakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel zitakabidhiwa rasmi utawala huo. Mji wa Quds (Jerusalem) ambao ni nembo ya ardhi, historia na dini ya Wapalestina mnamo Disemba mwaka 2018  ulikabidhiwa Israel kwa njia isiyo rasmi kufuatia uamuzi wa rais Trump kuhamishia ubalozi wa nchi yake mjini humo kutoka Tel Aviv.

Riyadh Mansour, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema kwa matazamo wa Wapalestina, mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne unapendelea Israel kikamilifu. Ameongeza kuwa: "Mpango wa Muamala wa Karne, hautakuwa na faida yoyote kwa Wapalestina kwani msingi wake ni kutwaa kikamilifu ardhi zote zilizoghusubiwa na kuzikabidhi rasmi kwa Israel zambamba na kupinga kurejea wakimbizi Wapalestina katika ardhi zao za jadi."

Rais Trump wa Marekani na Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Israel

Mbali na hayo,  mpango wa 'Muamala wa Karne' hauhusu tu Israel kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina bali pia unahusu kuipokonya Palestina uwezo wa kijeshi na kujihami. Kwa mujibu wa duru za habari, katika muamala huo wa karne uliowasilishwa na Marekani, nchi ndogo ya Palestina itakayoundwa haitakuwa na haki ya kuwa na jeshi wala silaha.

Hassan Hanizadeh, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anafafanua zaidi kuhusu kadhia hii kwa kusema: "Silaha pekee ambazo Wapalestina wataruhusiwa kuwa nazo ni silaha ndogo ndogo ambazo hutumiwa na polisi. Wanataka Ghaza isiyo na hatari wala silaha na kwa muda mrefu wamekuwa wakitafakari kuhusu mpango huo.

Kipengee hicho cha Muamala wa Karne kinawasilishwa katika hali ambayo utawala wa Kizayuni unamiliki silaha angamizi za nyuklia.

Mbali na hayo, mpango huo unawasilishwa na Marekani na Utawala wa Israel wakati ambao utawala huo umepata pigo baada ya kushindwa kukabiliana na makombora ya makundi ya wanamuqawama wa Palestina katika vita vya hivi karibini vya siku mbili vya Oktoba mwaka 2018 na vita vya siku nne vya Mei 2019. Katika vita hivyo Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu alilazimika kukubali mapatano ya kusitisha vita baada ya kushindwa kukabiliana na wimbi la makombora ya makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina.

Kufichuliwa vipengee vipya vya mpango wa  'Muamala wa Karne' ambavyo vinawanyima Wapalestina haki ya kuwa na jeshi na silaha ni jambo ambalo limepelekea Wapalestina wote waungane katika kuupinga mpango huo wa kibaguzi. 

Kuhusiana na nukta hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetoa taarifa na kusema: "Mpango wa rais wa Marekani unaojulikana kama 'Muamala wa Karne' ni sehemu ya jitihada za kuupa sura ya kisheria mfumo wa ubaguzi wa rangi au apertheid katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu."

Askari wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina

Kabla ya hapo pia, harakati za Jihad Islami na Hamas zilikuwa zimependekeza kuundwe harakati moja kubwa ya Wapalestina wote kwa lengo la kukabiliana na 'Muamala wa Karne.'

Wakati huo huo makundi ya Wapalestina yamekuwa yakijitahidi sana kuzishawishi nchi za Kiarabu na Kiislamu ziupinge mpango huo wa Marekani. Kuhusiana na hili, Khaled al-Qaddumi , mwakilishi wa Hamas mjini Tehran amesisitiza kuwa, nchi za Kiarabu na Kiislamu na pia watetea uhuru kote duniani wanapaswa kuungana na Wapalestina katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa, nchi za Kiarabu na Kiislamu zinapaswa kutumia ushawishi wao wa kisiasa na kidiplomasia kuzuia utumiaji mabavu wa Marekani na jinai zake katika eneo.

Mashinikizo ya kigeni na upinzani mkali wa makundi ya Wapalestina katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni jambo ambalo limeilazimisha serikali ya Marekani kuahirisha uzinduzi wa 'Muamala wa Karne'. Kwa hivyo kuimarishwa mshikamano wa makundi ya Wapalestina na kuongezeka idadi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu zinazopinga 'Muamala wa Karne' ni nukta ambazo zinaweza kuipelekea Marekani isitishe uzinduzi wa mpango huo wa kibaguzi unaolenga kuliangamiza taifa la Palestina kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel.