Amir wa Qatar hatoshiriki kikao cha Makka
(last modified Thu, 30 May 2019 08:17:58 GMT )
May 30, 2019 08:17 UTC
  • Amir wa Qatar hatoshiriki kikao cha Makka

Amir wa Qatar amekataa ombi la mfalme wa Saudi Arabia la kufanya safari katika mji wa Makka na badala yake amemtuma Waziri wake Mkuu kumwakilisha huko Saudia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imetangaza kuwa Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani Amir wa nchi hiyo hatoshiriki kikao cha Makka bali Abdallah bin Hamad Al Thani Waziri Mkuu wa Qatar ndiye atakayehudhuria kikao hicho akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi hiyo. Kikao cha Makka ambacho kimeitishwa na Riyadh kwa ajili ya kuchunguza kile kilichotajwa kuwa matukio ya karibuni katika eneo likiwemo shambulio la ndege zisizo na rubani za Yemen dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudi Arabia na pia kushambuliwa meli kadhaa za mafuta katika bandar ya al Fujaira nchini Imarati kinafanyika leo. 

Bandari ya Fujaira nchini Imarati

Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe 5 Juni mwaka 2017 ziliituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi na kisha zikakata uhusiano wao na Doha. Nchi hizo aidha zilifunga mipaka yake ya nchi kavu, baharini na anga na kuipatia Doha orodha ya masharti 13 iyatekeleze kabla ya kuondolewa mzingiro wa nchi hizo dhidi yake. Baada ya kupitia miaka miwili sasa tangu kujitokeza hali hii ya mvutano; Qatar si tu kuwa haijakubali hali hii bali imepigana kwa ushindi vita hivyo vya heshima na nchi nne za Kiarabu khususan Saudi Arabia kwa kuendelea  kusisitiza juu  kujitawala na umoja wa ardhi ya nchi hiyo. 

 

Tags