Zarif: Imarati inajaribu kuwa Israel ya pili katika Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mahojiano na televisheni ya al Arabi kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unatumia mabilioni ya dola kununua silaha huku ukifanya jitihada za kujaribu kuwa Israel ya pili katika eneo.
Akizungumza jana usiku katika mahojiano maalumu na televisheni ya al Arabi, Muhammad Javad Zarif ameeleza kuwa kuna nchi mbili tatu za Kiarabu katika eneo ambazo zinaamini kwamba zinaweza kuimarisha ushirikiano wao kwa kuwa na uhusiano na Marekani lakini zinakosea zinapodhani kuwa zinaweza kununua usalama wao kutoka Marekani, kwa sababu silaha zote hizo zitatumika kufanikisha malengo ya Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa kamwe hatutatoa mwanya kwa Marekani kuwatwisha wananchi wetu vita vya upande mmoja na bila shaka vita hivyo vitakuwa na madhara kwa wote kwa sababu vita ni vita tu. Zarif ameashiria vikwazo vya Marekani dhid ya Iran na kueleza kuwa vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na rais wa Marekani dhidi ya Iran ni ugaidi; na Iran kamwe haitafanya mazungumzo na magaidi. Mahojiano kamili ya Zarif na televisheni ya al Arabi yanatazamiwa kutangazwa leo Jumatano.