'Muamala wa Karne' umetayarishwa na Marekani kwa maslahi ya Wazayuni
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) zimesema utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani unalenga kuangamiza taifa la Palestina kupitia 'Muamala wa Karne' ulio kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi.
Hayo yalisemwa Jumapili ya jana katika mkutano baina ya Waziri wa Usalama wa Taifa wa Iran Mahmoud Alavi na maafisa wa ngazi za juu wa Hamas mjini Beirut. Kwa mujibu wa taarifa hiyo walioshiriki katika mkutano huo ni Naibu Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas Saleh Al-Arouri, mwanachama wa Idara ya Kisiasa ya Hamas Hessam Badran, mkuu wa masuala ya kigeni katika Hamas Osama Hamdan na mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon Ahmed Abdulhadi.
Kwa mujibu wa tovuti ya Hamas, katika mkutano huo, pande mbili zimesisitiza kuwa, sera ambazo Marekani inazitekeleza zinabainisha wazi kuwa maamuzi ya kuunga mkono Israel ambayo yamechukuliwa na rais wa Marekani yanatazamiwa kuendelea kwa kuunga mkono hatua ya utawala wa Israel ya kujenga vitongoji zaidi vya walowezi wa kizayuni katika Ukingo wa Magharibi na minuko ya Golan.
Wamesema baadhi ya hatua ambazo Marekani imezichukua katika kuunga mkono utawala wa Kizayuni ni kuutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala huo na kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo.
Aidha pande mbili zimejadili kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Iran na Hamas na ulazima wa mashauriano ya mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto na hatari zinazotokana na sisitizo la Markenai la kutekeleza 'Muamala wa Karne' ambao umekataliwa na Wapalestina wote pamoja na mataifa ya eneo.
Aidha pande mbili zimejadili njia za kukabiliana na njama za Marekani na Wazayuni katika eneo hasa kuhusu kadhia ya Palestina.