Wapalestina waandamana kupinga mkutano wa 'Muamala wa Karne' Bahrain
Maefu ya wananchi wa Palestina jana Jumanne walijitokeza mabarabarani kushiriki maandamano ya kupinga mkutano wa kuzindua Muamala wa Karne ulionza jana katika mji mkuu wa Bahrain, Manama.
Katika maandamano hayo yaliyofanyika katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Wapalestina waliteketeza kwa moto vibonzo na picha za Rais Donald Trump wa Marekani.
Waandamanaji hao waliokuwa wamemiminika katika miji mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi walisikika wakipiga nara ya 'Palestina sio ya kuuzwa!'
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na Wapalestina hao yalikuwa na jumbe zinazosema: "Kuanzia Bahrain hadi Saudia, hatubabaishwi na mabilioni yenu."
Wananchi wa Palestina walioshiriki maandamano ya jana Jumanne, yaliyofanyika sambamba na kuanza mkutano wa Muamala wa Karne unaomalizika leo, wamelaani vikali mkutano huo wa Mamana, na kusisitiza kuwa kamwe hawataruhusu kurubuniwa kwa fedha, ili wauze kadhia ya Palestina na utambulisho wao.
Hapo jana Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammad Shtayyeh alisema Wapalestina hawataki sadaka bali wanadai haki zao za kuwa huru na kukomeshwa uvamizi wa Israel na udhibiti wa dola hilo haramu wa maisha na uchumi wao.
Alieleza hatua kadhaa zilizochukuliwa na serikali ya Donald Trump katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambazo amesema ni vita dhidi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa Israel, kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo unaokaliwa kwa mabavu, kufunga ofisi ya mwakilishi wa Palestina mjini Washington na kusimamisha misaada ya Marekani kwa raia wa Palestina ikiwa ni pamoja na misaada iliyokuwa ikitolewa na nchi hiyo kwa wakala wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.