Wazayuni waua watoto 16 wa Kipalestina
Kituo cha Haki za Binadamu cha Mizan kimetoa ripoti na kusema kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2019, wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeshaua shahidi watoto 16 wa Kipalestina kwa kuwapiga risasi kwa makusudi.
Kituo hicho kimesema katika ripoti yake ya leo Jumatano kwamba, katika kipindi cha miezi sita iliyiopita, zaidi ya watoto 1,200 wa Kipalestina wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni. Katika kipindi hicho, wanajeshi makatili wa Israel wamewatia mbaroni kidhulma watoto wadogo 17 wa Kipalestina.
Ni kawaida kwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kukanyaga bila kujali makubaliano ya kimataifa yakiwemo yale yanayosisitiza kulindwa haki za watoto wadogo. Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshambulia mara 17 shule na vituo vya matibabu vya Ukanda wa Ghaza huku madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani si tu yakinyamaza kimya, bali yanafikia hata kuuhamasisha utawala huo pandikizi na kudai kuwa eti ni haki ya Israel kujilinda.
Kituo cha Takwimu cha Palestina kwa upande wake kilisema kwa mnasaba wa mwaka wa 70 tangu Wazayuni waanze kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina maarufu kwa jina la "Siku ya Nakba" kwamba Wapalestina laki moja wameshauliwa shahidi na utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwaka 1948 hadi hivi sasa.