Maafisa 60 wa jeshi la Israel wataka kukomeshwa ubaguzi wa rangi
Maafisa 60 wenye asili ya Ethiopia wa jeshi la Israel wametoa wito wa kukomeshwa ubaguzi wa rangi katika muundo wa jeshi la utawala huo.
Televisheni ya Israel imetangaza kuwa, makumi ya maafisa weusi wa jeshi la utawala huo wamemwandikia barua mkuu wa vikosi vya jeshi la Israel, Aviv Kochavi wakimtaka achukue hatua za kukomesha ubaguzi na ubaguzi wa rangi unaoendelea kushika kasi zaidi katika muundo wa jeshi la utawala huo.
Barua hiyo imeashiria idadi kubwa ya askari wenye asili ya Afrika katika jeshi la Israel na kuutishia kwamba, iwapo matakwa yao hayatatekelezwa, wao wenyewe watachukua hatua za kufanya mabadiliko.
Mayahudi wa Ethiopia maarufu kwa jina la Mafalasha, waliorubiniwa kwenda katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, tangu tarehe 6 mwezi huu wa Julai wamekuwa wakifanya maandamano ya kalalamikia unyanyasaji na ubaguzi wanaofanyiwa na Wazayuni.

Maandamano hayo makubwa yaliyoambatana na fujo yalifanyika katika miji ya Tel Aviv, Hayfa, Ashdod na Ashkelon. Watu 60 walitiwa mbaroni na maafisa usalama wa Israel wakati walipokandamiza kikatili maandamano hayo.
Mayahudi wa Ethiopia maarufu kwa jina la Mafalasha, ni miongoni mwa makundi maskini zaidi ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Mayahudi hao walirubuniwa kuacha makazi yao huko Ethiopia na kwenda kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwa tamaa ya kupata maisha mazuri. Hata hivyo wananyanyaswa na kubaguliwa sana na wanahesabiwa kuwa ni raia wa daraja la tatu wa utawala wa Kizayuni.