Saudia yapinga mpango wa Hija "kuendeshwa kimataifa".
Mshauri wa Mfalme wa Saudi Arabia amepinga hatua yoyote ya kuanzisha kamati ya kimataifa kwa ajili ya uendeshaji masuala ya ibada ya Hija.
Khalid Al-Faisal, mshauri wa mfalme wa Saudia, ambaye pia ni Amiri wa eneo la Makka amesema: Utawala wa Aal Saud hautaruhusu shughuli za Hija ziendeshwe kisiasa.
Pendekezo la kutaka amali za ibada ya Hija ziendeshwe na kamati maalumu ya kimataifa ya Ulimwengu wa Kiislamu limetolewa miaka kadhaa sasa na nchi na duru tofauti za Kiislamu lakini limepingwa na viongozi wa utawala wa Saudi Arabia.
Miito mingi zaidi ya kutaka Hija iendeshwe na kamati ya kimataifa imetolewa baada ya mamlaka za utawala wa Aal Saud kukwamisha uingiaji, usafirishaji na utoaji hudumu za makazi kwa mahujaji kutoka Qatar na vile vile kutokana na vizuizi walivyowekewa mahujaji kutoka Iran, Yemen na Libya.
Wakati huo huo duru za Saudia zimetangaza kuwa umezuka moto kwenye hoteli waliyofikia mahujaji wa Palestina kutoka Ukanda wa Gaza iliyoko katika mji mtukufu wa Makka. Hadi sasa hakujatolewa ripoti kuhusu idadi ya watu waliofariki au kujeruhiwa kutokana na moto huo.../