Mahujaji zaidi ya milioni moja wawasili Saudia kwa ajili ya Hija
Waziri wa Hija na Umra wa Saudi Arabia amesema nchi hiyo imepokea mahujaji zaidi ya milioni moja, wageni wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu walioenda kutekeleza ibada ya Hija ya mwaka huu.
Kanali ya televisheni ya Al-Ekhbariya imemnukuu Mohammed al-Bijawi, Waziri wa Hija na Umra wa Saudia akisema hayo na kuongeza kuwa, "Hadi sasa tumepokea mahujaji 1,150,000 hapa Saudi Arabia kwa ajili ya Hija."
Al-Bijawi ameeleza kuwa, wimbi hilo la mahujaji kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya amali za Hija linajiri wakati huu ambapo maandalizi ya kuwapokea wageni zaidi yanaendelea.
Inakadiriwa kuwa mwaka huu, Saudi Arabia itapokea mahujaji zaidi ya milioni mbili, kiasi kwamba mashirika ya ndege ya nchi hiyo yameshatenga tiketi zaidi ya 1,200,000 kwa ajili ya mahujaji.
Viwanja sita vya ndege vya ndani ikiwa ni pamoja na Jeddah, Riyadh, Al-Dammam, Madinatul-Munawwara, Al-Taif na Yan'ba vitapokea ndege zitakazobeba mahujaji wa mwaka huu.
Habari zaidi zinasema kuwa, kwa mara kwanza tokea mwaka 2016, ndege iliyowabeba mahujaji imetokea Sana'a, mji mkuu wa Yemen kwenda Saudia, ishara ya kupungua msuguano baina ya Riyadh na Sana'a. Ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 277 iliondoka Sana'a saa mbili usiku wa jana.
Waziri wa Kazi wa Harakati ya Ansarullah, Ghaleb Mutlaq amesema ndege 200 zitahitajika kwa ajili ya kuwasafirisha Wayemen 24,000 waliotangaza azma zao za kwenda kuhiji mwaka huu.
Takwimu rasmi zinaonesha kuwa, Saudia mwaka jana 2022, iliwapokea mahujaji 899,999, ikilinganishwa na idadi ndogo ya 60,000 mwaka 2021, na 10,000 mwaka 2020 kutokana na janga la Corona.