UAE yasema imewashambulia magaidi wanaoungwa mkono na Saudia nchini Yemen
(last modified Sat, 31 Aug 2019 14:53:31 GMT )
Aug 31, 2019 14:53 UTC
  • UAE yasema imewashambulia magaidi wanaoungwa mkono na Saudia nchini Yemen

Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE au Imarati) imewataja mamluki wanaopata himaya ya Saudia Arabi huko kusini mwa Yemen kuwa ni magaidi, nukta ambayo inaashiria ufa mkubwa katika madola hayo mawili ya Kiarabu ambayo yamekuwa yakishirikiana na vita dhidi ya watu wa Yemen.

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imesema jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya 'wanamgambo magaidi'  kwa kutegemea taarifa za kijasusi.

Taarifa hiyo imesema oparesheni hiyo imetekelezwa kwa lengo la kukabiliana na makundi ya wabeba silaha wenye uhusiano na mitandao ya kigaidi.

Taarifa hiyo imetolewa masaa kadhaa baada ya wapiganaji wa kusini mwa Yemen wanaotaka eneo hilo lijitenge na ambao wanapata himaya ya UAE kuchukua udhibiti wa mji wa Aden na kuwatimua wanamgambo wanaosaidiwa na Saudia ambao ni watiifu kwa rais wa zamani wa Yemen Abd Rabbuh Mansur Hadi waliokuwa wameingia katika mji huo wa bandarani juzi.

Kambi ya Hadi imesema mashambulizi hayo ya ndege za kivita za UAE yameua au kujeruhi zaidi ya watu 300.

Tangu baada ya kuanzisha uvamizi na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015, Saudia na Imarati kila moja imekuwa ikidhibiti baadhi ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo na kuwatumia vibaraka na mamluki wao kwa ajili ya operesheni za kijeshi dhidi ya vikosi vya jeshi la Yemen.