Waziri wa Ulinzi wa Lebanon: Tutajibu shambulizi lolote litakalofanywa na Israel
Waziri wa Ulinzi wa Lebanon amesema kuwa, nchi hiyo itajibu shambulizi lolote litakalofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ardhi ya Lebanon na kwamba nchi hiyo hii leo ni imara zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Elias Bou Saab amesema kuwa Lebanon imekuwa ikiimarika na kupata nguvu zaidi kadiri ilivyotoka kwenye migogoro mbalimbali iliyokumbana nayo na suala hilo linaonekana zaidi chini ya kivuli cha wapiganaji wa Muqawama (Hizbullah), Rais imara wa Jamhuri na maafisa wa serikali walio makini; kwa msingi huo Waisraeli wanapaswa kupata ibra kutokana na uhakika huo.
Waziri wa Ulinzi wa Lebanon ameongeza kuwa, Rais wa Lebanon na maafisa wengine wa nchi hiyo hawayapi umuhimu mashinikizo ya kigeni na jambo pekee linalopewa umuhimu ni maslahi ya Lebanon.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Jumapili iliyopita ilitekeleza kivitendo ahadi iliyokuwa imetolewa na Katibu Mkuu wake, Sayyid Hassan Nasrullah, ya kujibu mashambulizi yaliyofanywa na Israel huko Lebanon na kutoa jibu kali kwa uchokozi huo.
Katika shambulizi hilo kali, wapiganaji wa Hizbullah wamemuangamiza kamanda wa jeshi la Israel huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuharibu gari la kijeshi la utawala huo sambamba na kuua au kujeruhi watu wote waliokuwamo.