Hamas yapongeza maamuzi ya Mahakama ya Ulaya
(last modified Sat, 07 Sep 2019 12:54:17 GMT )
Sep 07, 2019 12:54 UTC
  • Hamas yapongeza maamuzi ya Mahakama ya Ulaya

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imepongeza uamuzi wa Mahakama ya Ulaya wa kuondoa jina la harakati hiyo na brigedi za Izzuddin al Qassam, tawi la kijeshi la harakati hiyo katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Hazim Qasim, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS akisema jana kwamba, hatua hiyo ya Mahakama ya Ulaya ni nzuri na inabidi jina la HAMAS litolewe kwenye orodha zote zinazoituhumu kidhulma harakati hiyo.

Amesema, mapambano ya Wapalestina ya kupigania ukombozi wa ardhi zao ni haki yao kisheria na hayakinzani hata chembe na sheria za kimataifa.

Brigedi za Izzuddin Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Ameongeza kuwa, kuiweka HAMAS katika orodha ya makundi ya kigaidi ni dhulma na ni kinyume na uadilifu, kwani kinakwenda kinyume na haki ya kila taifa ya kupambana na wavamizi wa ardhi zao.

Msemaji huyo wa HAMAS ameongeza kuwa, harakati hiyo itaendelea na mapambano yake dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel hadi pale itakapokomboa ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo dhalimu.

Kwa upande wake, Khalid al Shouli, wakili wa harakati hiyo ya Kiislamu alisema jana kuwa, Mahakama ya Ulaya yenye makao yake huko Luxembourg imelitoa jina la HAMAS na tawi la kijeshi la harakati hiyo yaani Brigedi za Izzuddin al Qassam, katika orodha ya kimataifa ya makundi ya kigaidi. Ni wazi kuwa hatua hiyo haiwezi kuufurahisha hata kidogo utawala wa Kizayuni wa Israel na vibaraka wake.

Tags