Answarullah: Ndege zisizo na rubani zinazoishambulia Saudia, zinatengenezwa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56035-answarullah_ndege_zisizo_na_rubani_zinazoishambulia_saudia_zinatengenezwa_yemen
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen, amesema kuwa ndege zisizo na rubani za jeshi la nchi hiyo, zinatengenezwa na Wayemen ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 16, 2019 07:26 UTC
  • Answarullah: Ndege zisizo na rubani zinazoishambulia Saudia, zinatengenezwa Yemen

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa wa Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen, amesema kuwa ndege zisizo na rubani za jeshi la nchi hiyo, zinatengenezwa na Wayemen ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Abdul-Wahhab al-Mahbashi, amesema kuwa uwezo wa kiulinzi wa jeshi na kamati za wananchi nchini Yemen umeongezeka maradufu licha ya mzingiro wa kila upande iliowekewa nchi hiyo kutoka kwa muungano vamizi unaoongozwa na Saudia. Kwa mujibu wa duru za habari, uwezo wa ndege hizo zisizo na rubani za jeshi na kamati za wananchi wa Yemen, sasa zimekuwa changamoto kubwa kwa Saudi Arabia.

Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen ambayo inatoa kipigo kwa Saudia na washirika wake

Hii ni katika hali ambayo Jumamosi iliyopita, kikosi cha ndege zisizo na rubani kwa kushirikiana na kamati za wananchi, kilirusha ndege 10 zilizotengezwa na Wayemen, na kushambulia vituo vya kusafishia mafuta vya Buqayq na Khurais, vinavyomilikiwa na Shirika la Kitaifa la Mafuta la Saudia ARAMCO, suala ambalo limeibua hitilafu katika shughuli za uzalishaji mafuta nchini Saudia. Inafaa kuashiria kuwa, Saudia kwa kushirikiana na washirika wake, ilianzisha vita na mashambulizi makali dhidi ya taifa masikini la Yemen tangu mwezi Machi 2015, ambavyo hadi sasa vimesababisha maelfu ya raia wa kawaida kuuawa. Hata hivyo muqawama wa raia wa nchi hiyo, umeifanya Saudia na washirika wake kufeli katika vita hivyo.