Ansarullah: Mashambulizi yajayo dhidi ya Saudia yatakuwa makali zaidi
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeapa kutoa majibu makali zaidi na yanayoumiza dhidi ya Saudi Arabia iwapo muungano vamizi unaoongozwa na utawala wa Aal-Saud hautasitisha uvamizi wake, mzingiro na mauaji dhidi ya wananchi wa Yemen.
Kiongozi wa Ansarullah, Abdul-Malik al-Houthi amesema madhali Saudia inaendeleza mashambulizi yake dhidi ya taifa la Yemen, ijiandae kupokea mapigo zaidi ndani ya ardhi yake na waitifaki wake.
Huku akishiria kuhusu shambulizi la Septembe 14 dhidi ya vituo vya kusafisha mafuta vya Saudia, al-Houthi amebainisha kuwa, "Sasa baada ya kushindwa na kupata pigo, hawana budi kusitisha hujuma na uvamizi dhidi ya Wayemen."
Amesisitiza kuwa, vikosi vya Yemen vitazishambulia vikali ardhi za Saudia na wapambe wake, na majibu yajayo yatakuwa makali zaidi. Taarifa ya Ansarullah ni radiamali kwa hatua ya Marekani ya kutaka kutuma askari zaidi nchini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu, kuimarisha kile kilichotajwa kama mfumo wa ulinzi wa anga wa Riyadh.
Hii ni baada ya jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za wananchi wa nchi hiyo na katika kujibu hujuma na mashambulizi ya Saudia na pia mzingiro wa kila upande wa muungano vamizi dhidi ya taifa hilo masikini (Yemen), lilivishambulia vituo vya kusafisha mafuta vya Buqayq na Khurais vya Saudia Jumamosi ya wiki iliyopita.
Shambulizi hilo lilivuruga kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji mafuta za Riyadh, sambamba na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia mbali na kuporomoka kwa soko la hisa nchini Saudia.