Makundi ya Palestina katika njia ya umoja
Katika siku za hivi karibuni pamewasilishwa mpango wa kiubunifu wa makundi ya Palestina kwa ajili ya kufikiwa maridhiano na umoja wa kitaifa, ambao pia umepokelewa na makundi ya Kipalestina ikiwemo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (HAMAS).
Mpango huo wa makundi ya Palestina umebuniwa na makundi ya Harakati ya Jihadul-Islami, Mrengo wa Kidemokrasia kwa ajili ya Uhuru wa Palestina, Chama cha Watu wa Palestina, Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa, Harakati ya Swaiqah na mengineyo, ambapo nayo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu (HAMAS) imeupokea kwa mikono miwili mpango huo. Moja ya vipengee muhimu vya mpango huo wa kiubunifu wa makundi ya Palestina ni kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kufikia mwishoni mwa mwaka huu, suala ambalo ndilo hitajio la taifa la Palestina. Nukta muhimu ni hii kwamba, mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne ambao ni mpango wa ubaguzi wa rangi na ambao kimsingi ni chombo cha kudhamini maslahi ya utawala haramu wa Kizayuni, ambao katika mwaka mmoja na nusu uliopita umevuruga maelewano kati ya makundi ya Wapalestina, sasa mazingira yanayofaa yameandaliwa na hivyo kuyafanya makundi hayo yahisi hata zaidi umuhimu wa kuwepo umoja baina yao.
Katika uwanja huo, serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekata mawasiliano yake na Marekani kama ambavyo pia haifuatilii tena mazungumzo ya maridhiano na utawala khabithi wa Kizayuni. Hata kama kabla ya hapo, mpango wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina ulikuwa ukizungumziwa, huku ukishindwa kutekelezwa kutokana na ukwamishaji mambo wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Chama cha Fat'h kinachoongozwa na rais wa serikali hiyo Mahmoud Abbas. Hata hivyo inaonekana kwamba hivi sasa kwa kuzingatia mienendo ya uhasama ya Marekani na utawala haramu wa Kizayuni, hususan dhidi ya ardhi zote za Palestina, suala la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ni lenye kupewa mazingatio makubwa na Wapalestina. Moja ya vipengee vingine muhimu vya mpango huo wa kiubunifuu, ni kufanyika kwa uchaguzi jumuishi kufikia mwanzoni mwa kwaka ujao wa 2020. Uchaguzi wa mwisho wa Palestina ulifanyika mwaka 2006 ambapo harakati ya HAMAS iliibuka mshindi. Tangu mwaka 2006 hadi leo yaani kwa muda wa miaka 13, hakujawahi kufanyika uchaguzi mwingine ndani ya Palestina, katika hali ambayo suala la uchaguzi ni moja ya matakwa muhimu ya makundi ya kisiasa ya Palestina hususan makundi ya muqawama. Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika hotuba yake kwenye kikao cha 74 cha mwaka huu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA amesema kuwa, yupo tayari baada tu ya kurejea kwake Palestina, aitishe uchaguzi jumuishi katika taifa hilo. Matamshi hayo ya Abbas pia yamepokelewa na kuungwa mkono na harakati ya HAMAS.
Kiufupi tunaweza kusema kuwa, hotuba ya Rais Mahmoud Abbas katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ni aina fulani ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Chama cha Fat'h kukubali mpango wa kiubunifu wa makundi ya Kipalestina. Hata kama kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kufanyika uchaguzi ni matakwa mawili muhimu ya makundi ya Palestina ambayo yamesisitizwa katika mpango huo wa kiubunifuu, lakini masuala mengine muhimu kama vile kurejea nyumbani wakimbizi wa Palestina, hali mbaya ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za utawala katili wa Kizayuni na pia haki za wafanyakazi katika eneo la Ukanda wa Gaza, hayajatajwa katika mpango huo wa kiubunifu. Inaonekana kwamba sababu kuu ya masuala hayo muhimu kutozingatiwa katika mpango huo, ni juhudi kubwa zinazofanywa na makundi ya muqawama kwa ajili ya kuimarisha umoja na kujiepusha na tofauti baina yao. Ni wazi kuwa masuala hayo yataweza kufuatiliwa baada ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kufanyika uchaguzi mkuu huko Palestina. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya HAMAS akasema kuwa, licha ya kuwekwa kando kwa sasa baadhi ya mapendekezo kwenye mpango huo, lakini harakati hiyo inakubaliana kwa ujumla na mpango tajwa.