Harakati ya Ansarullah yawaachia huru mateka 350 wa vita vya Yemen
Kamati ya mateka ya harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa, harakati hiyo imewaachia huru mateka 350 wakiwemo mateka watatu raia wa Saudi Arabia ikiwa ni katika kutekeleza makubaliano ya amani ya Stockholm.
Abdulkadir Murtadha, mkuu wa kamati ya mateka ya harakati ya Ansarullah amewaeleza waandishi wa habari kuwa, mateka hao wameachiwa leo chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu.
Murtadha amebainisha kuwa, katika awamu hii, Ansarullah imekusudia kuwaachia huru mateka wote walionusurika kifo katika mashambulio ya anga yaliyofanywa mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ambayo yalilenga jela ya Dhamar walikokuwa wamewekwa mateka hao wa vita.
Mkuu huyo wa kamati ya mateka ya harakati ya Ansarullah ameongeza kuwa: Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu litashughulikia zoezi la kuwasafirisha na kuwarejesha makwao mateka hao.
Mwanzoni mwa mwezi Septemba, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia ulishambulia kituo kimoja katika mkoa wa Dhamar ulioko kusini magharibi mwa Yemen, ambapo baadaye ilikuja kubainika kuwa kituo hicho ni jela inayotumika kuhifadhi mateka wa vita.../