Ansarullah yaonya askari wa Marekani walioko Saudia; jifunzeni kwa Vietnam
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56591-ansarullah_yaonya_askari_wa_marekani_walioko_saudia_jifunzeni_kwa_vietnam
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen, Muhammad Ali al-Houthi ameitaka Marekani ijifunze kutokana na vita vilivyojiri huko Vietnam kuanzia mwaka 1954-1975 na kuisababisha Marekani maafa na hasara kubwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 13, 2019 08:02 UTC
  • Ansarullah yaonya askari wa Marekani walioko Saudia; jifunzeni kwa Vietnam

Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen, Muhammad Ali al-Houthi ameitaka Marekani ijifunze kutokana na vita vilivyojiri huko Vietnam kuanzia mwaka 1954-1975 na kuisababisha Marekani maafa na hasara kubwa.

Aidha ameitaka serikali ya Washington ijifunze kutokana na vita vyake visivyokuwa na umuhimu wowote katika nchi za Iraq na Yemen.

Kauli hiyo ya afisa wa ngazi za juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen inajiri baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kutoa taarifa ikitangaza kuwa, nchi hiyo itatuma Saudia wanajeshi na zana zaidi za kivita. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ijumaa iliyopita ya Oktoba 11, wanajeshi wapya 1800, mitambo miwili ya kurushia makombora ya Patriot, ngao moja ya ulinzi wa makombora aina ya THAAD na squadroni mbili za ndege za kivita aina ya F-15 zitatumwa huko Saudia. 

Ukarabati wa vituo vya mafuta vya Saudia vilivyoshambuliwa na Ansarullah Septemba 15

Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ameihutubu Marekani kuhusu tangazo hilo kwa kuiambia: "Vikosi vyenu vilivyotangulia, zana zenu za kivita na makamanda wenu waliokiri wazi kuwa Marekani inaua raia wa Yemen, hawakutubabaisha, sembuse hawa wapya?"

Ameongeza kuwa, kuongeza idadi ya wanajeshi na zana za kivita hakuzimi ari ya taifa la Yemen kusimama kidete dhidi ya wavamizi wanaoongozwa na Saudi Arabia, kwa baraka kamili na uungaji mkono wa Marekani na waitifaki wake.