Hamas: Kuendelea kutiwa mbaroni Wapalestina nchini Saudia ni jambo lisilokubalika
Mkuu wa Ofisi ya Uhusiano wa Kitaifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesisitiza kuwa kuendelea kukamatwa na kufungwa jela nchini Saudia raia wa Palestina ni jambo lisilokubalika. Amesema faili la kesi hiyo hadi sasa halijapiga hatua yoyote.
Akizungumza kwenye mahojiano na shirika la habari la Qods, Hossam Badran mwakilishi wa harakati ya Hamas amesema kuwa watu waliotiwa mbaroni nchini Saudi Arabia kama walivyo raia wengine wa Palestina wanapenda ardhi na malengo yao wanayopigania. Amesema wanataraji kwamba raia hao wa Palestina walioko jela nchini Saudi Arabia wataachiwa huru haraka iwezekanavyo.
Harakati ya Hamas miezi kadhaa iliyopita ilitangaza kuwa Saudi Arabia imewatia mbaroni Muhammad al Khidr mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa harakati hiyo na makumi ya Wapalestina wengine.
Hadi sasa Hamas imeshawaomba viongozi husika wa Saudi Arabia iwaachie huru al Khidr na Wapalestina wengine walioko jela nchini humo. Muhammad Nazal mwakilishi mwingine wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mwezi Septemba mwaka huu aliripoti kuhusu hali mbaya ya kiafya inayomkabili Muhammad al Khidr kiongozi wa Hamas ambaye alitolewa jela na kupelekwa hospitali kwa matibabu. Muhammad al Khidr ni mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Hamas ambaye anaishi nchini Saudi Arabia kwa karibu miaka 30.